MWONGOZO WA IDARA YA HUDUMA BINAFSI (Personal Ministries)
Na Mch. Msholla, D. M – Mkurugenzi Idara ya Huduma Binafsi ECT 2016:
HISTORIA
Historia ya Idara hii inarejea kikundi cha wanawake kilichoanzishwa mwaka 1869 kusini mwa mji wa Lancaster, Massachusetts kilichoitwa Vigilant Missionary Society. Kazi ya kikundi hicho ilipelekea Mch. S. N. Haskell kuanzisha “Tract and Missionary Societies” katika Konferensi mbalimbali za New England mwaka 1870. Vikundi hivi viliwaandikisha washiriki katika shughuli ya kugawa bure au kuuza vijizuu, magazeti, vitabu na machapisho ya nyakati maalum (Periodicals). Vikundi hivi pia vilifanya uinjilisti wa mtu kwa mtu kwa kuwatembelea watu, kwa mawasiliano ya barua na kusaidia wahitaji.
Mwaka 1874 Konferensi Kuu (GC) ilianzisha General Tract and Missionary Society ambayo baadaye iliitwa International Tract and Missionary Society. GC ilipoanzisha idara ya Uchapishaji mwaka 1901 ilibeba pia chama hicho. Mwaka 1913 chama hicho kilibadilishwa jina na kuitwa Home Missionary Branch of Publishing Department na Edith M. Graham akawa Katibu wake wa kwanza ili kuhimiza Uinjilisti wa Washiriki.
Mwaka 1918 “Home Missionary” ilifanywa kuwa idara inayojitegemea lengo likiwa ni kuleta uhamsho wa dini ya kweli katika Kanisa na kwenda nje kuishiriki na wengine kazi kubwa ikiwa ni kuwafundisha wanaume kwa wanawake kila mahali duniani kwenda nje ya maeneo yao kuongoa roho kwa ajili ya Kristo.
Mwaka 1966 Home Missionary Department ikawa Lay Activities Department (Idara ya Huduma za Washiriki). Mwaka 1985 ikawa Personal Ministries (Idara ya Huduma Binafsi) ili kuwezesha na kuunganisha washiriki kukamilisha kazi ya Utume wa Kanisa Ulimwenguni.
UTUME WA IDARA
Ni kutoa nyenzo (resources) na kufundisha washiriki wa Kanisa kuunganisha nguvu zao na za viongozi wa Idara na maofisa katika kutangaza ujumbe wa mwisho wa wokovu katika Kristo. Kusudi kuu la Idara ni kuandikisha kila mshiriki katika huduma hai ya kuongoa roho.
MALENGO:
- Idara ilianzishwa kwa kusudi kuu la kusimamia shughuli za kuongoa roho kanisani.
- Idara ipo ili kufundisha na kutangaza Injili ya Yesu Kristo, katika muktadha wa ujumbe wa malaika watatu wa Ufunuo 14: 6 – 12.
- Ili kutimiza lengo hili idara inaendelea kutangaza habari njema kwa kusudi la kuongoa, kutunza na kufundisha kwa ajili ya Yesu Kristo wanaume na wanawake wakubwa kwa vijana.
- Kubuni program na kuandaa vitendea kazi ili kusaidia maeneo yote ya kazi ambayo ukuaji wake ni dhahifu.
- Kuunganisha washiriki katika kushiriki na kukamilisha kazi ya kuongoa roho.
MBINU NA SHUGHULI YA KUONGOA ROHO:
- Mbinu hizo ni pamoja na uinjilisti wa nyumba kwa nyumba,
- Kugawa machapisho mbali mbali kwa watu
- Mafundisho ya Biblia ya mtu mmoja mmoja.
- Mahubiri ya walei – ni pamoja na mafundisho ya Biblia ya mtu kwa mtu na mahubiri ya hadhara, uinjilisti wa magereza na miradi maalum ya huduma kwa jamii
- Kupanga na kuendesha shughuli za huduma kwa jamii zikihusisha vyama vya AMO na DORKASI katika kugawa vyakula, nguo, Elimu ya watu wazima, utoaji wa huduma ya kwanza, huduma ya kukuza malezi nyumbani, kusaidia katika majanga, nk.
- Kupanga na kusimamia ukusanyaji wa sadaka ya mavuno – mamilioni wamefikiwa na kuandikishwa katika masomo ya Biblia kwa njia ya posta, kukusanya pesa kwa ajili ya hospitali, shule, huduma kwa jamii na kukuza uinjilisti ulimwenguni
- Kusimamia mafundisho ya Shule ya Biblia kwa njia ya Posta.
- Kusaidiana na Shule ya Sabato kupanga na kuendesha vikosi vya shule ya Sabato.
- Kupanga na kusimamia huduma ya vikosi vidogo vidogo (Small Group Ministries).
- Kugawa machapisho (Literature Distribution) – ikihusisha kugawa nyumba kwa nyumba, kwa njia ya posta na kuhazimisha vitabu toka maktaba za makanisa mahalia
MUUNDO NA VIONGOZI WA IDARA:
Kiongozi huchaguliwa na Kanisa mahalia ili kuongoza katika kufundisha na kuelekeza Kanisa katika huduma hai ya kushuhudia. Kiongozi ndiye mwenyekiti wa baraza la idara
Ni jukumu lake kutoa taarifa kwa Kanisa na Halmashauri juu ya ushuhudiaji wa Kanisa.
Mwito Muhimu:
Mashujaa wa Agano Jipya walikuwa Wainjilisti wakiiga kazi ya Yesu ya kuokoa waliopotea, mfano, Mwanamke kisimani, Zakayo, nk.
Ndivyo walivyofanya akina Petro, Paulo,Barnabas, Filipo, Timotheo, Yohana Marko, nk.
Kiongozi wa Idara ameitwa katika urithi huo anaposhughulika kusimamia shughuli za kushuhudia za kanisa mahalia
Kiongozi wa Idara:
- Atafanya kazi bega kwa began a Mchungaji wa Kanisa au Mtaa.
- Ni mjumbe wa baraza la Kanisa.
- Wafuatao wanaleta taarifa zao kwa Kiongozi wa Idara ya huduma binafsi: Kiongozi wa Huduma kwa Jamii (AMO & DORKASI), Mratibu wa Usikivu, Kiongozi wa Mafundisho ya Biblia, Kiongozi wa Sadaka ya Mavuno, Kiongozi wa Magazeti ya Utume, Kiongozi wa Huduma za Magereza, na wengine wanaoshughulika na huduma za ushuhudiaji.
- Ni jukumu la kiongozi kuwasaidia kufanikiwa katika kazi yao na wote kusaidia katika ukuaji wa Kanisa.
- Ni jukumu lake kushirikiana na Waratibu wa Vikosi vya Shule ya Sabato ili kuhimiza na kutia moyo vikosi kutenda kama timu za ushuhudiaji.
- Anatakiwa awe na muda kupanga mipango ya kanisa ya kushuhudia na kukutana na baraza lake kwa ajili ya shughuli hai za uongoaji roho.
WAJIBU WA KIONGOZI:
Kushirikiana na Wainjilisti wa Kujitolea
- Ni muhimu kiongozi kujua kuwa watendakazi wa huduma za ushuhudiaji Kanisani ni wa kujitolea
- Ni jukumu lake kuwatafuta, kuwafundisha na kusimamia kazi yao.
- Wanaojitolea hufanya yale wanayopendelea au waliyohamasika kufanya na wala si lazima yale wanayolazimishwa kufanya kwa kutumia mimbari.
- Kuwabembeleza au kuwafanya wajione hatia hakusaidii kuwapa hamasa.
- Kukutana na mtu binafsi kwafaa sana kuliko mahubiri ya hadhara.
- Kuunda timu ya kusaidiana ni muhimu sana kwa ufanisi wa kazi.
- Kiongozi atafanya kazi na watu wachache takribani asilimia kumi, na ni kazi kubwa kupata idadi hii ya washiriki.
Kumbuka washiriki wanaojitolea wanahitaji:
- Kupewa kazi rasmi za kufanya na maelekezo sahihi.
- Wingi wa watu wa kutumia ili kufikia malengo yaliyo kusudiwa.
- Mrejesho mfupi na sahihi kwa yale waliyofanya.
- Kutambuliwa na kushukuriwa.
- Muda mfupi wa kuwa madarakani.
Kupanga
- Ni jukumu la kiongozi kusaidia viongozi wengine kuwa na mipango ya ushuhudiaji na uongoaji roho.
- Ni jukumu lake kukutana na viongozi muhimu ili kuweka magoli.
- Tafadhali kiongozi fanya magoli kuwa shirikishi kwa viongozi wenzako kanisani
- Elewa magoli mengi yanachanganya washiriki.
- Kanisa lapaswa kuwa na goli moja au mawili au matatu ya kushuhudia kwa wakati mmoja (miaka 2 au 3).
Elimu na Mawasiliano
- Ni lengo la kwanza kuhakikisha kila mshiriki anafahamu kwamba yupo kanisani kwa kusudi la kushuhudia.
- Kila mshiriki ni Mmishenari kwa familia yake, wafanyakazi/wafanya biashara wenzake, majirani zake, watu anaokutana nao kila siku kwa kupenda au la, nk.
- Ni kazi yake kuwatia moyo washiriki kutumia kila fursa na karama zao walizopewa na Bwana kutimiza mapenzi yake.
- Ni muhimu kuwakumbusha mara kwa mara washiriki juu ya wajibu wao wa kushuhudia.
Kusimamia Programu
- Ni msimamizi mkuu wa shughuli za Uinjilisti za Kanisa mahalia na ratiba ya kiulimwengu.
- Kila mradi wa Uinjilisti ni mchakato na si goli.
- Hupaswi kujisikia kushindwa ikiwa mradi haukufanikiwa.
- Ikiwa njia Fulani haikufaa, nyingine itafaa.
- Lengo/goli ni kuokoa wanaume kwa wanawake kwa ajili ya Ufalme wa Mungu.
Mambo Muhimu kwa Kiongozi:
- Awe Mtu wa Maombi
- Hakuna kinachohitajika zaidi katika kazi zaidi ya mahusiano halisi na Mungu.
- Ni lazima kuonyesha kila siku kwamba tumetulia kwa Yesu.
- Mahusiano na Mungu yatabadili tabia na maisha yetu
- Ili litaonyesha kwa wengine kwamba tumekuwa pamoja na Mungu (MH p. 512).
- Awe Mtu wa Imani
- Mtumishi wa Mungu anahitajika kuwa mtu wa imani kwa Mungu.
- Mungu anajali kazi za watu wake naye huleta viumbe wa mbinguni kushirikiana nao katika kazi.
- Unaposhindwa kuamini ahadi zake alizoahidi, na kudhani kuwa Yeye hawajali watumishi wake ni kumkosea na kutomheshimu Muumba wetu (CS pp. 233, 234).
- Awe Mtu Jasiri
- Kuwa na tumaini na kutokata tamaa ni vitu muhimu katika utumishi mkamilifu wa kazi ya Mungu
- Kukata tamaa ni dhambi na si kitu cha kuweka maanani (PK p. 164)
- Ujasiri, nguvu na uvumilivu ni vya muhimu kuwa navyo kazini (GW p. 39).
- Awe Mtu wa Vitendo
- Kazi ya Mungu inahitaji watu wanaoona upesi na kutenda haraka na kwa wakati, tena kwa nguvu.
- Kama ukisubiri kupima na kuondoa kila changamoto na kila mashaka, utafanya kidogo sana au hutafanya chochote kabisa..
- Ni afadhali wakati Fulani kufanya makosa katika kutenda kuliko kukaa tu katika mashaka na kutofanya chochote au kukaa kwa kusitasita na kukosa msimamo (3T p. 497)
WAJIBU WA KATIBU WA HUDUMA:
- Hujihusisha na uagizaji wa vitendea kazi vyote vya huduma za uinjilisti.
- Ni mwandishi na mtunzaji wa kumbukumbu za huduma kwa jamii, uongoaji roho, program za huduma za familia, vijana na watoto, Elimu ya uwakili, nk.
- Ni katibu wa baraza la Idara ya huduma binafsi. Hivyo anapaswa kutunza miuhtasri ya vikao hivyo.
- Ni mjumbe wa baraza la Kanisa.
- Anatenda kazi yake chini ya Mchungaji wa Kanisa/Mtaa na kiongozi wa idara ya huduma binafsi.
- Anapaswa kushirikiana na viongozi wa Idara ya Shule ya Sabato.
- Anashirikiana na Kiongozi wa idara ya Huduma Binafsi katika kubuni na kuandaa program za utume katika Kanisa lake mahalia.
Majukumu yake Maalum:
- Ni katibu wa baraza la Huduma na mtunza kumbukumbu za shughuli za utume.
- Ni mwandishi na mtuma taarifa kwenda kwa Mchungaji au Konferensi kila robo.
- Ni mtoaji wa taarifa ya shughuli za ushuhudiaji kwa baraza la Kanisa na Halmashauri ya Kanisa
- Ni mnunuzi wa machapisho ya uinjilisti na mtunzaji wa risti zote za manunuzi.
- Ulijulisha Kanisa juu ya uwepo na upatikaji wa zana za kazi ya uinjilisti
- Kupanga tarehe za utoaji kwa ajili ya kuunga mkono kazi za idara kwa mahitaji yasiyokidhiwa na bajeti ya Kanisa.
- Kuandika na kutunza kumbukumbu/taarifa za kazi na huduma zilizofanywa na washiriki na kutuma nakala kwa Mchungaji wa Kanisa/Mtaa ama kwa Mkurugenzi wa konferensi kwa wakati
- Kuandaa kabati la kutunzia vifaa vya uinjilisti. Ni muhimu kupanga vifaa vizuri ili iwe rahisi kwa wengine kuvipata ikiwa hayupo.
- Ni muhimu aweke daftari la kusahini wanaochukua vifaa. Ni kosa kuzuia viongozi wengine kupata vifaa kwa matumizi. Elewa kazi yako ni ya huduma na si ya kudhibiti na kuzuia matumizi ya vifaa kwa kazi ya Injili.
- Ni jukumu lake kununua vifaa vya washiriki kwa kuchukua idadi ya mahitaji na kununua vifaa hivyo kama vitabu, machapisho kwa ajili ya washiriki binafsi – jambo hili linategemea utaratibu wa konferensi husika.
KUHAMASISHA WASHIRIKI KUSHUHUDIA:
Agizo kuu la kwenda ulimwenguni mwote kwa kusudi la injili ni sehemu ya wajibu wetu kwa Mungu:
Agano Jipya
- Kanisa lilikuwa na kuongezeka haraka (Matendo 1: 15)
- Waongofu wapya 3000 kwa siku (Matendo 2: 41, 42, 47)
- Waongofu 5000 kwa siku (Matendo 4: 4)
- Na wengine wengi (Matendo 21: 20)
Kwa nini Kanisa lilikuwa kwa kasi
- Ni kwa sababu kila mmoja alijihusisha na ushuhudiaji
- “Kazi ya mungu haitamalizika mpaka wanaume na wanawake wanaokiri imani yetu waingie kazini na kuunganisha nguvu zao na za wachungaji na maofisa wa Kanisa” (GW uk. 352)
- Washiriki wanahitaji kuelimishwa, “Hapatakiwi kuchelewa katika mpango wa kuelimisha washiriki” (9T uk. 119)
Kwa nini watu wengi hawajihusishi na ushuhudiaji?
Kuna sababu nyingi zinazofanya watu wasijihusishe na kazi ya kuongoa roho, lakini sababu kuu sita ni hizi zifuatazo:
- Kutojiamaini (Lack of self confidence)
- Viongozi kutowatambua washiriki
- Washiriki kutokuombwa kufanya: Baadhi ya wachungaji na wazee wa makanisa wanafurahi kufanya kazi zote pekee yao na hivyo kutokubali kuwapa wengine majukumu. Kuna wengi ambao wangejihusisha kama wangeombwa kufanya hivyo.
- Ukosefu wa mafunzo: Washiriki wengi wangejitoa kufanya kama wangefundishwa jinsi ya kuanza (CS uk. 59). Mafundisho ni ya muhimu sana ili kuwawezesha watu kushiriki katika shughuli za ushuhudiaji.
- Uelewa mdogo wa wajibu huu kwa washiriki: Baadhi ya washiriki wanadhani kuhubiri na kufundisha ni kazi ya wachungaji. Wanadhani kazi yao ni kuja tu Kanisani na kutoa sadaka. Kudhani kwamba kazi yote itafanywa na wachungaji ni kosa kubwa (CS uk 68).
- Hakuna motisha: kwa kujua kwamba washiriki ni jeshi kubwa na lenye nguvu katka kumaliza kazi ya Mungu, ni muhimu sana kwamba “Makanisa yote yawe vituo vya mafunzo ya uinjilisti. Washiriki wafundishwe namna ya kuendesha mafundisho ya Biblia, madarasa ya lesoni, kusaidia wahitaji na wagonjwa. Wajifunze na kufanya kazi kwa vitendo kupitia kwa wakufunzi wenye uzoefu” (CS p. 59)
KUUNGANISHA JUHUDI ZA WASHIRIKI:
Kanisa ni wakala wa Mungu kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu. Lilianzishwa kwa ajili ya wokovu wa wanadamu wote. Kiongozi wa Idara ya Huduma Binafsi wanawajibika kuhakikisha kila mshiriki anashiriki katika kazi hii muhimu ya kuongoa roho kwa ajili ya Kristo.