Mafundisho Makuu ya Imani ya Waadventista Wa Sabato

Kanisa la Waadventista Wa Sabato linaikubali Biblia kama tamko lao pekee la imani na inayashikilia Mafundisho fulani Makuu ya Imani kuwa ndiyo Mafundisho ya Maandiko Matakatifu. Imani hizi kama zilivyoelezwa hapa, zinajumuisha uelewa wa kanisa na namna linavyoyaeleza mafundisho ya Maandiko. Mapitio ya Matamko haya yanaweza kutarajiwa kwenye kikao cha Mkutano Mkuu wa Kanisa la kiulimwengu wakati kanisa linapoelekezwa na Roho Mtakatifu kwenye uelewa ulio mkamilifu wa Kweli ya Biblia au inapopata lugha iliyo bora zaidi ya kuelezea mafundisho ya Neno Takatifu la Mungu.

1. Maandiko Matakatifu:

Maandiko Matakatifu, yaani Agano la Kale na Jipya, ndiyo Neno la Mungu lililoandikwa likatolewa kwa uvuvio wa Mungu, kupitia kwa watu watakatifu wa Mungu walionena na kuandika kama walivyoongozwa na Roho Mtakatifu. Ndani ya Neno hili Mungu amemkabidhi mwanadamu maarifa yaliyo ya lazima kwa ajili ya wokovu. Maandiko Matakatifu ni ufunuo thabiti wenye mamlaka wa mafundisho ya imani na kumbukumbu aminifu ya matendo ya Mungu katika historia.

(2 Petro 1:20, 21; 2 Tim. 3:16, 17; Zab. 119:105; Mith. 30:5, 6; Isa. 8:20; Yoh. 17:17; 1 Thess. 2:13; Waebr. 4:12.)

2. Utatu Mtakatifu:

Kuna Mungu mmoja: Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu, umoja wa Nafsi tatu za milele. Mungu hapatikani na mauti, mwenye nguvu zote, ajuaye yote, aliye juu ya yote, na aliyeko daima. Yeye hana mwisho na ni zaidi ya ufahamu wa kibinadamu, hata hivyo anafahamika kupitia kujifunua kwake Binafsi. Milele zote yu astahili kuabudiwa, kusujudiwa, na kutumikiwa na viumbe wote.

(Kumb. 6:4; Math. 28:19; 2 Kor. 13:14; Efe. 4:4-6; 1 Petro 1:2; 1 Tim. 1:17; Ufu. 14:7.)

3. Baba:

Mungu Baba wa milele ndiye Muumbaji, Chimbuko, Mtegemezaji na Mfalme wa viumbe vyote. Ni mwenye haki na mtakatifu, mwingi wa rehema, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, na mwingi wa uthabiti wa upendo na uaminifu. Tabia na uwezo vilivyodhihirishwa ndani ya Mwana na ndani ya Roho Mtakatifu pia ni ufunuo wa Baba.

(Mwa. 1:1; Ufu. 4:11; 1 Kor. 15:28; Yoh. 3:16; 1 Yoh. 4:8; 1 Tim. 1:17; Kut. 34:6, 7; Yoh. 14:9.)

4. Mwana:

Mungu Mwana wa milele alifanyika mwili katika Yesu Kristo. Kupitia kwake vitu vyote viliumbwa, tabia ya Mungu imefunuliwa, wokovu wa mwanadamu unakamilishwa na ulimwegu unahukumiwa. Milele zote Mungu kweli, alifanyika Mwanadamu kweli, Yesu aliye Kristo. Alichukuliwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na kuzaliwa na bikira Mariamu. Akaishi na kupitia uzoefu wa majaribu kama mwanadamu, lakini kwa ukamilifu alionyesha kwa mfano haki na upendo wa Mungu. Kwa miujiza yake alidhihirisha uwezo wa Mungu na alithibitishwa kama Masihi aliyeahidiwa. Aliteseka na kufa kwa hiari msalabani kwa ajili ya dhambi zetu, na kama mbadala wetu, alifufuliwa kutoka katika wafu, na akapaa kuhudumu katika hekalu la mbinguni kwa niaba yetu. Atakuja tena katika utukufu kwa ajili ya ukombozi wa mwisho wa watu wake na urejeshwaji wa vitu vyote.

(Yoh. 1:1-3, 14; Kol. 1:15-19; Yoh. 10:30; 14:9; War. 6:23; 2 Kor. 5:17-19; Yoh. 5:22; Luka 1:35; Fil. 2:5-11; Waeb. 2:9-18; 1 Kor. 15:3, 4; Waeb. 8:1, 2; Yoh. 14:1-3.)

5. Roho Mtakatifu:

Mungu Roho wa Milele alikuwa mtendaji pamoja na Baba na Mwana katika Uumbaji, kufanyika mwili, na katika ukombozi. Aliwavuvia waandishi wa Maandiko Matakatifu. Aliyajaza maisha ya Kristo na uwezo. Huwavuta na kuwasadikisha wanadamu; na wale wanaoitikia huwafanya upya na kuwabadilisha wawe na sura ya Mungu. Akitumwa na Baba na Mwana ili kuwa siku zote na watoto wake, hutoa karama za kiroho kwa kanisa, huliwezesha kumshuhudia Kristo, na kwa kupatana na Maandiko huliongoza kwenye ukweli wote.

(Mwa. 1:1, 2; Luka 1:35; 4:18; Mat. 10:38; 2 Petro 1:21; 2 Kor. 3:18; Efes. 4:11, 12; Mat. 1:8; Yoh. 14:16-18, 26; 15:26, 27; 16:7-13.)

6. Uumbaji:

Mungu ni Muumba wa vitu vyote, na amefunua katika Maandiko uhalisi wa tukio la shughuli zake za uumbaji. Katika siku sita Bwana alizifanya “mbingu na nchi” na vitu vyote vilivyo hai juu ya nchi, akastarehe siku ya saba ya juma lile la kwanza. Na hivyo akaanzisha Sabato kama kumbukumbu ya milele ya kukamilika kwa kazi yake ya uumbaji. Mwanaume na mwanamke wa kwanza walifanywa kwa mfano wa Mungu kama upeo wa kazi yake ya uumbaji, wakapewa utawala juu ya ulimwengu, na wakaagizwa kuwajibika na utunzaji wake. Wakati ulimwengu ulipomalizika kila kitu kilikuwa ni “chema sana,” kikitangaza utukufu wa Mungu.

(Mwa. 1; 2; Kut. 20:8-11; Zab. 19:1-6; 33:6, 9; 104; Waeb. 11:3.)

7. Asili ya Mwanadamu:

Mwanaume na mwanamke waliumbwa kwa mfano wa Mungu kila mmoja akiwa na nafsi yake, uwezo wake, na uhuru wake wa kufikiri na kutenda. Ingawa waliumbwa viumbe huru, kila mmoja ni muunganiko usiogawanyika wa mwili, akili, na roho, akimtegemea Mungu kwa uhai na pumzi na mengine yote. Wakati wazazi wetu wa kwanza walipomwasi Mungu, walikana utegemezi wao kwa Mungu na wakaanguka kutoka hadhi yao ya juu iliyokuwa chini tu ya Mungu. Sura ya Mungu iliyokuwa ndani yao ikaharibiwa na wakawa chini ya mauti. Wazao wao hushiriki asili hii ya anguko na matokeo yake. Wanazaliwa wakiwa na udhaifu na mivuto ya kuelekea kwenye uovu. Lakini Mungu katika Kristo aliupatanisha ulimwengu na nafsi yake, na kwa njia ya Roho wake hurejesha ndani ya wanadamu watubuo sura ya Muumba wao. Wakiwa wameumbwa kwa ajili ya utukufu wa Mungu, wanaitwa kumpenda na kupendana wao kwa wao, na kutunza mazingira yao.

(Mwa. 1:26-28; 2:7; Zab. 8:4-8; Mat. 17:24-28; Mwa. 3; Zab. 51:5; War. 5:12-17; 2 Kor. 5:19, 20; Zab. 51:10; 1 Yoh. 4:7, 8, 11, 20; Mwa. 2:15.)

8. Pambano Kuu:

Jamii yote ya wanadamu sasa inahusika katika pambano kuu baina ya Kristo na Shetani lihusulo tabia ya Mungu, sheria yake, na ukuu wake juu ya ulimwengu. Pambano hili lilianzia mbinguni wakati kiumbe aliyeumbwa na kutunukiwa uhuru wa kuchagua, katika kujiinua akawa Shetani, mpinzani wa Mungu, na kuwaongoza kwenye uasi sehemu ya malaika. Alianzisha roho ya uasi katika ulimwengu huu pale alipowaongoza Adamu na Hawa kuingia dhambini. Dhambi hii ya mwanadamu ilisababisha uharibifu wa sura ya Mungu katika wanadamu, uvuragaji wa mpangilio wa ulimwengu ulioumbwa, na mwishowe kuteketea wakati wa gharika iliyoikumba dunia hii. Ukitazamwa na ulimwengu wote ulioumbwa, ulimwengu huu ukawa uwanja wa vita wa malimwegu yote, ambao kutokana na vita hiyo Mungu wa upendo hatimaye atathibitika kuwa mwenye haki. Ili kuwasaidia watu wake katika pambano hili, Kristo anamtuma Roho Mtakatifu na malaika watiifu kuwaongoza, kuwalinda, na kuwategemeza katika njia ya wokovu.

(Ufu. 12:4-9; Isa. 14:12-14; Eze. 28:12-18; Mwa. 3; War. 1:19-32; 5:12-21; 8:19-22; Mwa. 6-8; 2 Petro 3:6; 1 Kor. 4:9; Waeb. 1:14.)

9. Maisha, Kifo, na Ufufuo wa Kristo:

Katika maisha ya Kristo ya utii mkamilifu kwa mapenzi ya Mungu, mateso yake, mauti, na ufufuo, Mungu alitoa njia pekee ya kafara kwa ajili ya dhambi ya mwanadamu, ili wale ambao kwa imani wanapokea upatanisho huu waweze kuwa na uzima wa milele, na ulimwengu wote uweze kuelewa vizuri zaidi upendo mtakatifu na usio na ukomo wa Muumbaji. Kafara hii kamilifu huthibitisha haki ya sheria ya Mungu na fadhili za tabia yake; kwa kuwa hufanya yote mawili; kuhukumu dhambi yetu na kutupatia msamaha. Kifo cha Kristo ni cha mbadala na cha kulipia, cha kupatanisha na cha kubadilisha. Ufufuo wa Kristo hutangaza ushindi wa Mungu dhidi ya nguvu za uovu, na kwa wale wanaopokea kafara hujihakikishia ushindi wao wa mwisho dhidi ya dhambi na mauti. Hutangaza Ubwana wa Yesu Kristo, ambaye mbele yake kila goti la mbinguni na duniani litapigwa.

(Yoh.  3:16; Isa. 53; 1 Petro 2:21, 22; 1 Kor. 15:3, 4, 20-22; 2 Kor. 5:14, 15, 19-21; War. 1:4; 3:25; 4:25; 8:3, 4; 1 Yoh. 2:2; 4:10; Kol. 2:15; Waf. 2:6-11.)

10. Uzoefu wa Wokovu:

Katika upendo usio na ukomo na rehema zake Mungu alimfanya  Kristo, asiyejua dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili kwamba katika yeye tuweze kufanywa haki ya Mungu. Tukiongozwa na Roho Mtakatifu tunatambua hitaji letu, tunakiri hali yetu ya kuwa wenye dhambi, tunatubu maasi yetu, na kuonesha imani katika Yesu kama Bwana na Kristo, kama Mbadala na Kielelezo. Imani hii inayopokea wokovu huja kupitia katika uwezo wa kimbingu wa Neno na ni karama ya neema ya Mungu. Kupitia kwa Kristo tunahesabiwa haki, tunafanywa kuwa wana na binti za Mungu, na kukombolewa kutoka katika hali ya kuwa chini ya dhambi. Kupitia kwa Roho tunazaliwa upya na kutakaswa; Roho hufanya upya nia zetu, huandika sheria ya Mungu ya upendo katika mioyo yetu, na tunapewa uwezo wa kuishi maisha matakatifu. Tukikaa ndani yake, tunakuwa washirika wa asili ya Uungu na tuna hakika ya wokovu sasa na katika hukumu.

(2 Kor. 5:17-21; Yoh. 3:16; Wag. 1:4; 4:4-7; Tito 3:3-7; Yoh. 16:8; Wag. 3:13, 14; 1 Petro 2:21, 22; War. 10:17; Luk. 17:5; Mark 9:23, 24; Waef. 2:5-10; War. 3:21-26; Kol. 1:13, 14; War. 8:14-17; Wag. 3:26; Yoh 3:3-8; 1 Petro 1:23; War. 12:2; Waeb. 8:7-12; Eze. 36:25-27; 2 Petro 1:3, 4; War. 8:1-4; 5:6-10.)

11. Kukua katika Kristo:

Kwa kifo chake msalabani Yesu alizishida nguvu za uovu. Yeye aliyewatiisha pepo wachafu wakati wa huduma yake hapa duniani, amezivunja nguvu zao na kuthibitisha kuwa mwisho wao ni uangamivu usioepukika. Ushindi wa Yesu hutupatia ushindi dhidi ya nguvu za uovu ambazo bado zinatafuta kututawala, tunapotembea naye kwa amani, furaha, na uhakika wa upendo wake. Sasa Roho Mtakatifu anakaa ndani yetu na kututia nguvu. Tukidumu kujikabidhi kwa Yesu kamaBwana na Mwokozi wetu tunawekwa huru kutoka katika mzigo wa matendo yetu yaliyopita. Hatuishi tena gizani, katika hofu ya nguvu za uovu ujinga na katika kukosa maana kwa namna ya maisha yetu ya awali. Katika uhuru huu mpya ndani ya Kristo, tumeitwa kukua katika kufanana na tabia yake, tukiongea naye kila siku katika sala, na kujilisha Neno lake, tukilitafakari Neno lake na majaliwa yake, tukiimba sifa zake, tukikusanyika pamoja kwa ajili ya ibada, na kushiriki katika utume wa kanisa. Tukijitoa katika kuwahudumia kwa upendo wale wanaotuzunguka na katika kuwashuhudia wokovu wake; kuwepo kwake nasi daima kwa njia ya Roho hugeuza kila wasaa na kila kazi kuwa uzoefu wa kiroho. 

(Zab. 1:1, 2; 23:4; 77:11, 12; Kol 1:13, 14; 2:6, 14, 15; Luk. 10:17-20; Waef. 5:19, 20; 6:12-18; 1 Wath. 5:23; 2 Petro 2:9; 3:18; 2 Wak. 3:17, 18; Waf. 3:7-14; 1 Wath. 5:16-18; Math. 20:25-28; Yoh. 20:21; Wag. 5:22-25; War. 8:38, 39; 1 Yoh. 4:4; Waeb. 10:25.)

12. Kanisa:

Kanisa ni jamii ya waumini wanaomkiri Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi. Katika mwendelezo wa kufungamana na watu wa Mungu wa nyakati za Agano la Kale, tunaitwa kutoka duniani; na tunajiunga pamoja kwa ajili ya ibada, kwa ajili ya ushirika, kwa ajili ya mafundisho katika Neno, na kwa ajili ya adhimisho la Meza ya Bwana, kwa ajili ya huduma kwa wanadamu wote, na kwa ajili ya mbiu ya injili kwa ulimwengu wote. Kanisa linapata mamlaka yake kutoka kwa Kristo, ambaye ni Neno lililofanyika mwili, na kutoka katika Maandiko, ambayo ndiyo Neno lililoandikwa. Kanisa ni familiya ya Mungu; iliyofanywa naye kuwa watoto wake, huku washiriki wake wakiishi katika msingi wa Agano Jipya. Kanisa ni mwili wa Kristo, jamii ya wenye imani ambayo Kristo mwenyewe ndiyo kichwa. Kanisa ni bibi arusi ambaye Kristo alimfia ili apate kumtakasa na kumsafisha. Wakati wa kurudi kwake kwa ushindi, ataliwasilisha kwake mwenyewe kanisa lenye utukufu, waaminifu wa karne zote, walionunuliwa kwa damu yake, likiwa halina waa wala kunyanzi, bali likiwa takatifu na lisilo na ila.

(Mwa. 12:3; Mat. 7:38; Waef. 4:11-15; 3:8-11; Math. 28:19, 20; 16:13-20; 18:18; Waef. 2:19-22; 1:22, 23; 5:23-27; Wakol. 1:17, 18.)

13. Masalio na Utume wake:

Kanisa la kiulimwengu linajumuisha wale wote ambao wanamwamini Kristo kiukweli, ila katika siku za mwisho, kipindi cha kuenea kwa ukengeufu, masalio wameitwa kuzishika Amri za Mungu na Imani ya Yesu. Masalio hawa hutangaza kuwadia kwa saa ya hukumu, hutangaza wokovu kupitia Kristo, na hupiga mbiu ya kukaribia kwa marejeo yake ya pili. Tangazo hili huwakilishwa na mfano wa malaika watatu wa Ufunuo 14; nayo huambatana na kazi ya hukumu mbinguni isababishayo kazi ya toba na matengenezo duniani. Kila muumini ameitwa kuwa na sehemu binafsi katika ushuhuda huu uendao ulimwenguni kote.

(Ufu. 12:17; 14:6-12; 18:1-4; 2 Kor. 5:10; Yuda 3, 14; 1 Petro 1:16-19; 2 Petro 3:10-14; Ufu. 21:1-14.)

14. Umoja katika mwili wa Kristo:

Kanisa ni mwili mmoja ulio na washiriki wengi, walioitwa kutoka kila taifa, kabila, lugha, na jamaa. Katika Kristo tu viumbe vipya; kubaguana kwa rangi, tamaduni, elimu, na utaifa, na tofauti baina ya tabaka la juu na la chini, tajiri na maskini, mwanamme na mwanamke, havipaswi kutuletea mgawanyiko katikati yetu. Sote tu sawa katika Kristo, ambaye kwa Roho mmoja ametufunga katika ushirika mmoja pamoja naye na sisi wenyewe kwa wenyewe; tunapaswa kutumika na kutumikiwa pasipo upendeleo au kusitasita. Kupitia kwa ufunuo wa Yesu Kristo katika maandiko tunashiriki imani na tumaini moja, na tunawafikia wote kwa ushuhuda mmoja. Umoja huu una chimbuko lake katika umoja wa Mungu mmoja mwenye nafsi tatu  ambaye ametufanya sisi kuwa watoto wake.

(War. 12:4, 5; 1 Kor. 12:12-14; Math. 28:19, 20; Zab. 133:1; 2 Kor. 5:16, 17; Mat. 17:26, 27; Wag. 3:27, 29; Kol. 3:10-15; Waef. 4:14-16; 4:1-6; Yoh. 17:20-23.)

15. Ubatizo:

Kwa njia ya ubatizo tunakiri imani yetu katika kifo na ufufuo wa Yesu Kristo kuwa bwana na mwokozi, tunakuwa watu wake na tunapokelewa kama washirika wa kanisa lake. Ubatizo ni mfano wa muunganiko wetu pamoja na  Kristo, msamaha wa dhambi zetu, na kupokea kwetu Roho Mtakatifu. Ni kwa kuzamishwa majini na unategemea uthibitisho wa imani katika Yesu na ushahidi wa toba ya dhambi. Unafuatia mafunzo katika Maandiko Matakatifu na ukubali wa mafundisho yake.
(War. 6:1-6; Kol. 2:12, 13; Mat. 16:30-33; 22:16; 2:38; Math. 28:19, 20.)

16. Meza ya Bwana:

Meza ya Bwana ni ushirika katika mfano wa mwili na damu ya Yesu kama udhihirisho wa imani katika Yeye, Bwana na Mwokozi wetu. Katika uzoefu huu wa ushirika Kristo anakuwepo kukutana na kuwaimarisha watu wake. Kadri tunavyoshiriki kwa furaha, tunatangaza mauti ya Bwana hadi arudipo tena. Maandalizi kwa ajili ya Meza ya Bwana hujumuisha kujihoji nafsi, toba, na ungamo. Bwaa aliamuru huduma ya kutawadhana miguu kuimarishwa kutakaswa upya, kuonyesha nia ya kutumikiana wenyewe kwa wenyewe katika unyenyekevu ufafanao na wa Kristo, na kuungaa mioyo yetu katika upendo. Huduma ya Meza ya Bwana ni wazi kwa waumini wote wakristo.

(1 Kor. 10:16, 17; 11:23-30; Math. 26:17-30; Ufu. 3:20; Yoh. 6:48-63; 13:1-17.)

17. Karama za Kiroho na Huduma:

Mungu hukirimia washiriki wote wa kanisa lake katika kila kizazi karama za kiroho ambazo kila mshiriki atatumia katika huduma ya upendo kwa ajili ya mema ya kawaida ya kanisa na wanadamu. Zikitolewa na uwakala wa Roho Mtakatifu, ambaye humgawia kila mshiriki kama apendavyo mwenyewe, karama hizo hutoa uwezo wote na huduma zinazohitajiwa na kanisa katika kutekeleza shughuli zake zilizoamriwa na Mungu. Kulingana na Maandiko, karama hizi hujumuisha huduma kama imani, uponyaji, unabii, mahubiri, mafundisho, utawala, usuluhishi, huruma, na huduma ya kujitolea kwa ajili ya kusaidia na kuwatia moyo watu. Baadhi ya washiriki huitwa na Mungu na kukirimiwa na Roho kwa shughuli zinazotambuliwa na kanisa kwenye uchungaji, uinjilisti, utume, na huduma za kufundisha hasa zile zinazohitajika katika kuwapatia washiriki zana kwa ajili ya huduma, kulijenga kanisa hadi ukomavu wa kiroho, na kukuza umoja wa imani na maarifa ya Mungu. Pale washiriki wanapozitumia karama hizi za kiroho kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu, kanisa hulindwa dhidi ya mivuto miharibifu ya mafundisho ya uwongo, na hukua kwa ukuaji unaotoka kwa Mungu, na hujengeka imara katika imani na upendo.

(War. 12:4-8; 1 Kor. 12:9-11, 27, 28; Waef. 4:8, 11-16; Mat. 6:1-7; 1 Tim. 3:1-13; 1 Petro 4:10, 11.)

18. Karama ya Unabii:

Mojawapo ya karama za Roho Mtakatifu ni unabii. Karama hii ni alama inayolitambulisha Kanisa la Masalio na ilidhihirishwa katika huduma ya Ellen G. White. Kama mjumbe wa Bwana, maandishi yake ni chimbuko la ukweli endelevu na wenye mamlaka ambao hulipatia kanisa faraja, uongozi, maelekezo, na maonyo. Pia yanaweka wazi kwamba Biblia ndiyo kipimo ambacho kutokana nacho mafundisho yote na uzoefu ni lazima vipimwe.

(Yoeli 2:28, 29; Mat. 2:14-21; Waebr. 1:1-3; Ufu. 12:17; 19:10.)

19. Sheria ya Mungu:

Kanuni kuu za sheria ya Mungu zimetiwa pamoja katika Amri Kumi na mfano wake ulidhihirishwa katika maisha ya Kristo. Zinadhihirisha upendo wa Mungu, mapenzi yake, na makusudi yake kuhusiana na mwenendo wa binadamu na mahusiano na zinawahusu watu wote katika kila kizazi. Amri hizi ndizo msingi wa Agano la Mungu na watu wake na kipimo kwenye hukumu ya Mungu. Kupitia uwakala wa Roho Mtakatifu zinasonda dhambi na kuamsha hisia za uhitaji wa Mwokozi. Wokovu wote ni kwa neema na si kwa matendo, lakini tunda lake ni utii kwa Amri Kumi. Utii huu hukuza tabia ya kikristo na kuleta matokeo ya hali ya ustawi. Ni ushahidi wa upendo wetu kwa Bwana na wajibu wetu kwa wanadamu wenzetu. Utii wa imai hudhihirisha uwezo wa Kristo katika kubadilisha maisha, na hivyo kuimarisha ushuhuda wa Kikristo.

(Kut. 20:1-17; Zab. 40:7, 8; Math. 22:36-40; Kumb. 28:1-14; Math. 5:17-20; Waeb. 8:8-10; Yoh. 15:7-10; Waef. 2:8-10; 1 Yoh. 5:3; War. 8:3, 4; Zab. 19:7-14.)

20. Sabato:

Muumbaji mkarimu, baada ya siku sita za Uumbaji, alipumzika siku ya saba na kuizindua Sabato kwa ajili ya watu wote kama kumbukumbu ya Uumbaji. Amri ya nne ya sheria za Mungu zisizobadilika inaagiza utunzaji wa Sabato hii ya siku ya saba kama siku ya mapumziko, ibada, na huduma, kwa kupatana na mafudisho na uzoefu wa Yesu, aliye Bwana wa Sabato. Sabato ni siku ya mawasiliano yenye furaha na Mungu na baina yetu sisi wenyewe kwa wenyewe. Ni ishara ya ukombozi wetu katika Kristo, alama ya utakaso wetu, dalili ya utii wetu, na mwonjo wa umilele wetu wa siku zijazo katika ufalme wa Mungu. Sabato ni ishara ya daima ya Mungu ya agano lake la milele baina yake na watu wake. Utunzaji wenye furaha wa wakati huu mtakatifu toka jioni hata jioni, jua kucha hadi jua kuchwa ni adhimisho la matendo ya Mungu ya uumbaji na ukombozi.

(Mwa. 2:1-3; Kut. 20:8-11; Luka 4:16; Isa. 56:5, 6; 58:13, 14; Math. 12:1-12; Kut. 31:13-17; Eze. 20:12, 20; Kumb. 5:12-15; Waeb. 4:1-11; Walawi. 23:32; Marko 1:32.)

21. Uwakili:

Tu mawakili wa Mungu, tuliokabidhiwa na Yeye wakati na fursa, uwezo na mali, na mibaraka ya dunia pamoja na rasilimali zake. Tunawajibika kwake kwa matumizi sahihi ya vitu hivyo. Tunakiri umilikaji wa Mungu kwa njia ya kutoa huduma ya uaminifu kwake na kwa wanadamu wenzetu, na kwa kurudisha zaka na kutoa sadaka kwa ajili ya utangazaji wa injili Yake na kwa kutegemeza ukuaji wa kanisa Lake. Uwakili ni upendeleo uliotolewa kwetu na Mungu kwa ajili ya malezi ya upendo na ushindi dhidi ya choyo na tamaa. Wakili hufurahia mibaraka inayowajia wengine kama matokeo ya uamiifu wake. 

(Mwa. 1:26-28; 2:15; 1 Nyak. 29:14; Hagai 1:3-11; Mal. 3:8-12; 1 Cor. 9:9-14; Math. 23:23; 2 Kor. 8:1-15; War. 15:26, 27.)

22. Mwenendo wa Mkristo:

Tumeitwa kuwa watu watauwa wanaofikiri, wanaohisi, na wanaotenda kulingana na kanuni za mbinguni. Ili Roho aumbe upya ndani yetu tabia ya Bwana wetu tunapaswa kujihusisha tu katika mambo yale ambayo yatazaa usafi, afya, na furaha vifananavyo na vya Kristo, katika maisha yetu. Hii inamaanisha kwamba starehe na maburudisho yetu vinapaswa kufikia viwango vya juu vya maonji na uzuri wa Kikristo. Huku tukitambua tofauti za kiutamaduni, mavazi yetu yanapaswa kuwa ya kawaida, ya mtindo usio wa zamani sana au wa karibuni sana, na nadhifu, yawastahilio wale ambao uzuri wao wa kweli hautokani na mwonekano wao wa nje bali ni mapambo yasiyoharibika yenye roho ya upole na utulivu. Pia inamaanisha kwamba kwa kuwa miili yetu ni mahekalu ya Roho Mtakatifu, tunapaswa kuitunza kwa akili. Pamoja na kuwa na mazoezi na mapumziko ya kutosha, tunapaswa kuchagua vyakula vyenye afya zaidi kadri inavyowezekana na kuepuka vyakula vilivyo najisi, vilivyotajwa kwenye Maandiko Matakatifu. Kwa kuwa vinywaji vya vileo, tumbaku, matumizi mabaya ya madawa na madawa ya kulevya hudhuru miili yetu, yatupasa kuepukana navyo pia. Badala yake tunapaswa kujishughulisha na chochote kifanyacho mawazo na miili yetu kuwiana na Kristo, anayetamani uzima wetu, furaha yetu, na wema wetu. 

(War. 12:1, 2; 1 Yoh. 2:6; Waef. 5:1-21; Filp. 4:8; 2 Kor. 10:5; 6:14-7:1; 1 Petro 3:1-4; 1 Kor. 6:19, 20; 10:31; Lawi. 11:1-47; 3 Yoh. 2.)

23. Ndoa na Familia:

Ndoa ilizinduliwa na Mungu kule Edeni na kuthibitishwa na Yesu kuwa ni muunganiko wa maisha yote baina ya mwanaume na mwanamke walio katika mahusiano ya upendo. Kwa wakristo, kifungo cha ndoa ni kwa Mungu na baina yao wenyewe kwa wenyewe na inapaswa kuingiwa tu baina ya washirika wawili walio kwenye imani moja. Kupendana, kuheshimiana, kustahiana ni nyuzi nyuzi za mahusiano haya, zinazopaswa kuakisi upendo, utakatifu, ukaribu na udumishwaji wa mahusiano baina ya Kristo na kanisa lake. Kuhusu talaka, Yesu alifundisha kwamba mtu amwachaye mwenzi isipokuwa kwa sababu ya uasherati na akaoa au kuolewa na mwingine azini. Ingawaje baadhi ya mahusiamo ya kifamilia yaweza kushindwa kufikia viwango, wenzi katika ndoa ambao wamejitoa kikamilifu kila mmoja kwa mwezake katika Kristo wanaweza kufikia umoja wenye upendo kupitia uongozi wa Roho na malezi ya kanisa. Mungu hubariki familia na hukusudia kwamba wanafamilia wasaidiane wao kwa wao kufikia ukomavu mkamilifu. Wazazi wawalee watoto wao katika kumpenda na kumtii Bwana. Kwa kielelezo chao na maneno yao wawafundishe kwamba Kristo ni mtiishaji mweye upendo, daima mpole na mweye kujali, anayetaka wawe viungo vya mwili wake, familia ya Mungu. Ukaribu wa kifamilia unaoongezeka ni mojawapo ya alama za ujumbe wa mwisho wa injili. 

(Mwa. 2:18-25; Math. 19:3-9; Yoh. 2:1-11; 2 Kor. 6:14; Efe. 5:21-33; Math. 5:31, 32; Marko. 10:11, 12; Luka. 16:18; 1 Kor. 7:10, 11; Kut. 20:12; Waeb. 6:1-4; Kumb. 6:5-9; Mith. 22:6; Mal. 4:5, 6.)

24. Huduma ya Kristo katika hekalu la mbinguni:

Kuna hekalu mbinguni, hema la kweli lililosimamishwa na Bwana na siyo mwanadamu. Ndani yake Kristo anahudumu kwa niaba yetu, akiwezesha kupatikana kwa ajili ya waumini fanaka za kafara yake ya upatanisho iliyotolewa mara moja msalabani kwa ajili ya wote. Alizinduliwa kuwa Kuhai wetu Mkuu na akaanza huduma yake ya uombezi wakati wa kupaa kwake mbinguni. Mnamo mwaka 1844, mwishoni mwa kipindi cha unabii wa siku 2,300, aliingia katika awamu ya pili na ya mwisho ya huduma yake ya upatanisho. Ni kazi ya hukumu ya upelelezi ambayo ni sehemu ya mwisho ya huduma yake ya upatanisho. Ni kazi ya hukumu ya upelelezi ambayo hatimaye itakomesha dhambi yote, iliyokuwa mfano wa kutakaswa kwa hekalu la kale la Waebrania katika Siku ya Upatanisho. Katika huduma hiyo kielelezo hekalu lilitakaswa kwa damu ya wanyama wa kafara, lakini mambo ya mbiguni hutakaswa kwa kafara kamilifu ya damu ya Yesu. Hukumu ya upelelezi hufunua kwa viumbe wa mbinguni ni nani miongoni mwa wafu wamelala katika Kristo na hivyo, katika Yeye wanahesabiwa kustahili kuwa na sehemu katika ufufuo wa kwanza. Pia inadhihirisha wazi ni nani miongoni mwao walio hai wanakaa ndani ya Kristo, wakiishika Amri za Mungu na imani ya Yesu, na katika Yeye hivyo basi, wako tayari kwa kuhamishwa kuingia katika ufalme wake wa milele. Hukumu hii huthibitisha haki ya Mungu katika kuwaokoa wale wanaomwamini Yesu. Hutangazwa kwamba wale waliodumu kuwa watiifu kwa Mungu watapokea ufalme. Hitimisho la huduma hii ya Kristo itakuwa ndiyo mwisho wa kufungwa kwa mlango wa rehema ya wanadamu kabla ya Marejeo ya Yesu.

(Waeb. 8:1-5; 4:14-16; 9:11-28; 10:19-22; 1:3; 2:16, 17; Dan. 7:9-27; 8:13, 14; 9:24-27; Hes. 14:34; Eze. 4:6; Law. 16; Uf. 14:6, 7; 20:12; 14:12; 22:12.)

25. Kuja kwa Kristo mara ya pili:

Kuja kwa Kristo mara ya pili ndilo tumaini lenye baraka la kanisa, hitimisho kuu la Injili. Kuja kwa Mwokozi kutakuwa halisi, binafsi, kutakakoonekana, na kwa dunia nzima. Atakaporudi wenye haki waliokufa watafufuliwa na pamoja na weye haki walio hai watavikwa utukufu na kuchukuliwa kwenda mbinguni, lakini waovu watakufa. Kutimizwa karibu kabisa kwa sehemu nyigi za unabii, pamoja na hali ya sasa ya ulimwengu, huoyesha kwamba kuja kwa Kristo ku karibu sana. Wakati wa tukio hilo haukufafauliwa, na hivyo basi tunahimizwa kuwa tayari kwa nyakati zote. 

(Tito 2:13; Waeb. 9:28; Yoh. 14:1-3; Mat.1:9-11; Math. 24:14; Uf. 1:7; Math. 24:43, 44; 1 Thess. 4:13-18; 1 Kor. 15:51-54; 2 Thess. 1:7-10; 2:8; Uf. 14:14-20; 19:11-21; Math. 24; Marko13; Luka 21; 2 Tim. 3:1-5; 1 Thess. 5:1-6.)

26. Mauti na Ufufuo:

Mshahara wa dhambi ni mauti. Lakini Mungu ambaye peke yake hapatikani na mauti, atawapa uzima wa milele waliokombolewa wake. Mpaka siku hiyo mauti ni hali ya kutokuwa na fahamu kwa watu wote. Wakati Kristo aliye uzima wetu, atakapotokea, wenye haki waliofufuliwa na wenye haki walio hai watavikwa utukufu na kunyakuliwa juu ili kumlaki Bwana wao. Ufufuo wa pili ambao ni ufufuo wa waovu, utatokea miaka elfu moja baadaye. 

(War. 6:23; 1 Tim. 6:15, 16; Maomb. 9:5, 6; Ps. 146:3, 4; Yoh. 11:11-14; Kol. 3:4; 1 Kor. 15:51-54; 1 Thess. 4:13-17; Yoh. 5:28, 29; Uf.  20:1-10.)

27. Miaka elfu moja na mwisho wa dhambi:

Milenia ni miaka elfu moja ya utawala wa Kristo pamoja na watakatifu wake mbinguni kati ya ufufuo wa kwanza na wa pili. Wakati huo waovu waliokufa watahukumiwa; dunia itakuwa ukiwa na utupu, bila wanadamu wakazi walio hai, lakini ikikaliwa na shetani na malaika zake. Mwishowe Kristo na watakatifu wake na mji Mtakatifu, watashuka duniani kutoka mbinguni. Ndipo waovu waliokufa watafufuliwa, nao pamoja na shetani na malaika zake watauzigira mji; lakini moto kutoka kwa Mugu utawateketeza na kuitakasa dunia. Na Na hivyo ulimwengu utakuwa huru bila dhambi na weye dhambi milele.

(Uf. 20; 1 Kor. 6:2, 3; Yer. 4:23-26; Uf. 21:1-5; Mal. 4:1; Eze. 28:18, 19.)

28.Nchi Mpya:

Katika dunia mpya, ambamo haki hukaa, Mungu ataweka tayari makao ya milele kwa waliokombolewa na mazingira makamilifu kwa maisha ya milele, upendo, furaha, na kujifunza mbele yake. Kwa kuwa hapa Mugu mweyewe atakaa pamoja na watu wake, na taabu na mauti zitakuwa zimepita. Pambano litakuwa limemalizika, na dhambi haitakuwepo tena. Vitu vyote vyenye uhai na visivyo na uhai vitatangaza kwamba Mugu ni pendo; naye atatawala milele. Amina. 

(2 Petro 3:13; Isa. 35; 65:17-25; Math. 5:5; Uf. 21:1-7; 22:1-5; 11:15.)