Juma la Maombi la
Idara ya Huduma za Familia
Somo la Watoto
Umuhimu wa Neno la
Mungu
Masomo ya Juma la Maombi
3 – 10 November 2018
MASOMO YA WATOTO
KUTAFUTA HAZINA KATIKA NENO LA MUNGU
Mfahamu Mtunzi
Julie Weslake
Amekua mwalimu na pia mkurugenzi wa idara ya huduma za watoto divisheni ya Pasifiki kusini. Amekua mwenye hamu ya makanisa na familia mbalimbali kujenga imani ndani ya watoto.
UTANGULIZI
Biblia ni kama hazina yenye thamani. Tunapojifunza biblia juma hili pamoja tutajifunza mafungu pamoja katika juma hili yatakayotufundisha juu ya:
Hazina iliyopo ndani ya Biblia.
Kuitegemea Biblia
Kuchunguza maneno yake
Kuitumia biblia maishani
Kumuona Yesu
Kuelewa matumaini
Jema na baya
Faraja
Yote hayo yatatupatia HAZINA katika BIBLIA.
SABATO YA KWANZA
Novemba 03, 2018
KWA NINI TUITHAMINI BIBLIA
Fungu: 20bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi;
21kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako. (mathayo 6:20-21)
Jemma alitengeneza boksi dogo la pekee na kulipamba na picha mbalimbali.alitamani kumpa bibi yakekwa kuwa alimpenda sana bibi yake. Jemma alifahamu pa kuliweka. Aligundua ni wapi bibi anatunza hazina yake, hivyo basi alikwenda na kuweka kandokando ya hazina ya bibi na picha ambazo bibi hupendelea kutazama.
Katika rafu ama shelfu kulikua na kitabu. Jemma alitafakari kuwa hiki chaweza kuwa kitabu cha pekee cha bibi yake kwa kuwa kilikuwa katika shelfu ya pekee. Alipokifungua alishangazwa sana maana kuna mtu ambaye alikuwa ameandika ndani yake kwa kupigia mistari baadhi ya sentensi na maneno. Jemma alijua kuwa hapaswi kamwe kuandika ama kuchora ndani ya vitabu, na hivyo akamuuliza bibi yake kwa nini aliandika na kuchora ndani ya kitabu chake hicho cha pekee.
Bibi yake alimueleza kuwa kitabu hicho kilikuwa cha pekee mno.Kilikua kinaitwa BIBLIA.Bibi alimueleza kuwa alikuwa anakisoma kila siku. Maneno yaliyopo ndani yake hususan yale aliyoyapigia mstari yalikua hazina kubwa ambayo alipenda ayakumbuke maana yalimuunganisha na Yesu na upendo wake kwake. Bibi alimueleza kuwa maneno yale yalimuonesha namna ya kumpenda Yesu. Jumbe za kitabu hicho yalimpa madhumuni ya siku na matumaini ya wakati ujao. Bibi yake alimueleza kuwa hawezi kuishi bila kusoma jumbe ambazo Mungu amempatia kila siku kupitia kitabu hiki.
Jemma alifurahi. Yeye pia alihitaji kumpenda Yesu na kujifunza zaidi habari zake. Alihitaji maneno haya ambayo ni hazina yafanye maisha yake kuwa na furaha. Hivyo basi alimuomba bibi yake amfundishe namna ya kusoma biblia na kuielewa ili aishi na Yesu kama rafiki wake wa karibu.
Bibi alifurahi sana. Alisema hakuna jambo la muhimu kama kujifunza maneno yaliyopo kwenye BIBLIA. Alisema kuwa Biblia ni kama kuwa na ramani ya thamani, na kuwa ukitumia muda wako kusoma biblia, ni kama kuchimba lulu na dhahabu, au vito vya thamani.
19 Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba;
20bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi;
21kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako. (mathayo 6:19-21) katika mafungu haya , Yesu anatushauri tusitumie muda mwingi katika maisha yetu kujaribu kutafuta mali ya ulimwengu huu. Tunapaswa kutumia muda wetu na fedha zetu katika mambo ambavyo Yesu angependa tuvifanye ili hazina yetu iwe mbinguni. Kwa kuwa ilipo hazina yetu ndipo ilipo mioyo yetu.
Katika hadithi inayopatikana katika Mathayo 13:44-46 Yesu aliwaambia wanafunzi wake “44 Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile.
45 Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri;
46 naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua.”
Unaweza kupenda kuuza kila ulichonacho ili ununue hilo shamba ili tu upate hazina hiyo. Furaha ya kuwa na Yesu na kuishi naye milele ni kitu cha thamani sana. Ili tufike mbinguni tutafurahi kuachana na vyote katika maisha yetu na kutumia muda mwingi kusoma Biblia.
Jadili
Unaweza ukatumia fedha zako na muda wako katika nini ili upate hazina inayotolewa na biblia?
Omba
Muombe Mungu akusaidie utafute hazina muhimu katika neno lake unazohitaji ili uishi maisha matakatifu. Mshukuru kwa hazina aliyokupa tayari.
Tengeneza
Chora ramani ya thamani kwa ajili ya chumba chako, kanisa au nyumbani. Ficha mafungu ya Biblia kisha yaonyeshe katika ramani yako ya thamanini wapi yanapatikana. Ikiwa rafiki zako wameyapata na wana familia yako, yasomeni pamoja.
JUMAPILI
Novemba 04, 2018
SOMA BIBLIA: INAWEZA KUAMINIWA.
Fungu: 15na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu.
16 Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; (2Timotheo 3:16)
Bibi alimuonesha Jemma palipoandikwa kuwa Biblia ni kitabu cha Mungu. Kinaitwa maandiko matakatifu kwa kuwa yanaelezea habari za Mungu na namna ya kumpa mioyo yetu na kuishi kwa ajili yake. Bibi alielezea kuwa Biblia sio kitabu kimoja bali ni maktaba ya vitabu 66 – vilivyoandikwa na watu tofautitofauti baada ya Mungu kuwapa maneno ya kuandika. Watu aliandika kile walichokikumbuka miaka mingi iliyopita, na wengine waliandika juu Yesu alipokuwa duniani. Wengine wameandika nyimbo au mashairi na wengine wameandika juu ya Vitu ambavyo vingefanyika katika wakati ujao.
Biblia hutuambia kuwa ujumbe uliopo kwenye biblia hautokani na mawazo tu ya waandishi. “21 Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.”
Kitabu kimoja katika Biblia hutuambia juu ya kujana aitwaye Timotheo ambaye aligundua hazina ya biblia. Aligundua biblia kupitia kwa mama yake Yunisi, na bibi yyake Loisi. Walijua yalivyo ya thamani maneno ya biblia na kuamua kukaa na timotheo kila siku na kumfundisha namna ya “kuchimba katika hazina” ya biblia na kutoa moyo wake kwa Yesu.
Kwa kuwa biblia ilivuviwa na Mungu mwenyewe, timotheo alikuwa na imani kwa Yesu kiasi kwamba alipata ujasiri wa kumshuhudia Yesu na kuwaongoza watu wengine kuishi kwa ajili ya Yesu.
Wathesalonike walimuamini Sila na Timotheo walipowaambia juu ya Hazina ya biblia na wakaachana na ibada ya miungu na kuanza kumpenda Yesu, Mungu anayeishi.Paulo alimtukuza Mungu kwa ajili ya hili.aliwaandikia wathesalonike akisema “13 Kwa sababu hiyo sisi nasi twamshukuru Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini.” (1 wathesalonike 2:13)
Bibi alimuuliza Jemma ikiwa anajua anachopaswa kukitumainia. Jemma alijibu kuwa ni kama kuamini kuwa baba atamdaka alipomuambia aruke ndani ya sehemu yenye kina kirefu ya kisima cha kuogelea.
Bibi alimwambia kuwa kusoma biblia, kuamini maneno ya biblia, kulitokana na Mungu; kisha kutenda kikuamricho ni kama kusoma na kufuata maelekezo ya mapishi unayoamini kuwa ulichokichanganya kitatokea kile kile ulichokua umekusudia kiwe.
Jadili
Ni vitabu gani ulivyosoma na program zipi ulizoziona na kungundua kuwa sio za kweli? Ni vitabu gani ulivyonavyo na program ulizonazo zilizo halisi na za kweli?
Omba
Muombe Mungu akusaidie ujielekeze katika hadithi za bibliazitakazokusaidia ukue vizuri kiroho kuliko hadithi zisizo za kweli huku zinafurahisha.
Tengeneza
Panga viti katika chumba kwa namna ambayo utaweza kuweka kikwazo njiani. Andika maelekezo ya mtu kusoma ili kumsaidia mtu aliyefungwa kitambaa machoni aweze kuvuka kikwazo katika kutembea kwake humo kwa mfano andika, andika hatua zilizobaki ili kumaliza mwendo, hatua ngapi kulia au mbele wanazotakiwa kuchukua ili wafike mwisho salama.
JUMATATU
Novemba 05, 2018
KUCHUNGUZA BIBLIA – NAMNA
FUNGU: “14 Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee.”
Jemma alimueleza bibi juu ya wakati ambapo alikuwa na mama yake akitembelea hifadhi lakini hawakupata ni wapi ndege walihifadhiwa. Iliwalazimu wasimame na kuanza kuangalia ramani ya hifadhi ili iwaongoze katika njia sahihi. Ilichekesha sana maana pamoja na kuwa walizunguka sana, hifadhi ya ndege ilikuwa dakika 5 tu kutoka pale walipokuwa kwa ktembea kwa mguu.
Bibi alicheka na kusema ni kama watu wamtafutao Mungu na kusudi lake na furaha kwa ajili ya maisha yao. Wakati Fulani wanatafuta kila mahali kumbe Mungu yupo karibu nao tu. Wanachohitaji ni kusoma biblia tu. Wengi hudhani kuwa biblia ni ngumu sana kuisoma, kwamba haieleweki. Wakati mwingine hata hawaamini kuwa biblia ni neno la Mungu la kweli kwa ajil yao. Wakati mwingine wanadhani kuwa biblia imejaa tu sheria.
Njia njema ya kuanza kujifunza biblia ni kuomba. Roho wa Mungu atatusaidia kuelewa tunachokisoma. Yesu aliporudi mbinguni, aliahidi kuwa atatutumia “roho wa kweli” kuwa pamoja nasi milele. “17 ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.”
“26 Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.” (Yohana 14:17,26).
Mpendwa Yesu, tafadhali nisaidie leo nielewe ninachokisoma katika neno lako, BIBLIA.
Bibi alimueleza Jemma kuwa angetamani kama angempa miwani itakayomuwezesha kuona Mungu ni nani na anafananaje. Kama miwani hiyo ingekuwepo ingetunesha kuwa jambo la muhimu sana kuhusu Mungu ni kwamba anatupenda. Tunapoyaangazia maneno ya biblia tunapaswa kuvaa miwani iitwayo “Mungu ni pendo”. Ni rahisi kuuona upendo wa Mungu katika mafungu haya;
“16 Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.”
“19 Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza.” ( 1 Yohana 4:16,19)
kiini cha ujumbe wenye upendo juu ya Mungu ni kwamba alimtuma mwana wake Yesu kristo afe kwa ajili yetu: “9 Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu.”
Mungu anatupenda sana kiasi kwamba anatutafuta kama mchungaji amtafutavyo kondoo aliyepotea, na hawezi kuitafuta njia yake ya kurudi nyumbani. Mungu ni ramani ya thamani lakini pia ni Hazina.
Mpendwa Yesu, asante kwa kutupenda, pamoja na kuwa hatustahili. Hutusaidia kuuona upendo wako katika kila neno tunalosoma ndani ya biblia.
Jadili
Ni kwa njia zipi zingine waweza kupokea ujumbe wa biblia bila kusoma?
Omba
Muombe Mungu akuonyeshe mpango wake kwa ajili ya maisha yako unapojifunza neno lake kwa uaminifu.
Tengeneza.
Buni na kuandaa miwani maalumu ya “ Mungu ni pendo” kwa ajili ya kusoma biblia. Unaweza ukatengeneza kwa kutumia karatasi gumu ama waya laini kisha ukaandika maneno pembeni “Mungu ni pendo”.
JUMANNE
Novemba 06, 2018
KUTUMIA HAZINA YA MUNGU MAISHANI - BIBLIA HUNIONGOZA
FUNGU:” 5 Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.”
Jemma alipenda sana kuwatengenezea watu vitu na kusaidia kazi nyumbani na shuleni pia. Lakini wakati mwingine alikuwa hajisikii tu kusaidia kazi, na wakati mwingi alifikiri amefanya chaguzi zisizo sahihi wakati watu walipomuudhi au kumfanya ajisikie huzuni. Alisema alijitahidi sana lakini hakuweza kufanya badiliko lolote. Aliwaza kama hazina za biblia zinaweza kumfanya awapende watu zaidi na kumsaidia kufanya chaguzi sahihi.
Bibi alimhakikishia kuwa kila mtu hufanya makosa, nay a kuwa hazina tunazozipata ndani ya biblia zinaweza kuwa na msaada. Hazina ya kwanza ambayo tunapaswa kuikumbuka ni hii ya kwamba pamoja na kuwa hatuoni tofauti katika maisha tunapaswa kutokuacha kusoma biblia. Yesu aliwaambia wanafunzi wake kuwa inafanya kazi kama mzabibu. Mradi tu matawi yameng’ang’aniakatika shina ,yatadumu kuzaa matunda mema. (Yohana 15:5). Na hivyo basi kila siku tunapaswa kujiungamanisha na Yesu ili tuweze kuzaa matunda. Muunganiko huu unatuwezesha kutenda kama Yesu mwenyewe anavyotenda na kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wakatimzabibu unazaa matunda, wengine watafurahia kuyala pia. Tutakapozaa matunda ya hazina ya biblia, tunaweza kuwa Baraka kwa wengine.
Jemma alikumbuka hadithi moja katika biblia juu ya binti mdogo muisraeli aliyechukuliwa kama mtumwa na akamwambia bwana wake juu ya nguvu ya uponyaji ya Mungu alipokuwa anaumwa. Kwa kuwa alijali na kushiriki na wengine habari za neno la mungu alilokuwa nalo kutoka katika hazina ya biblia, bwana wake shujaa Naamani aliponywa. Unaweza kusoma habari hii katika 2 wafalme 5:1-14.
Bibi alimueleza kuwa kila jambo jema tunalolitenda linatoka kwa Yesu, na kwamba tunapaswa kumshukuru kwa kutusaidia. “3 Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote;
4 atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu.”
Jemma alitamani sana kuwa kama Yesu. Bibi alimueleza kuwa, kuwa kama Yesu ni zoezi la maisha, nan i katika kusoma kutoka katika hazina na kuomba ndipo tunakua hatua kwa hatua. “18 Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho.” (2 wakorintho 3:18)
Unganishwa na Yesu kupitia kulisoma neno lake, naye atakupa moyo wake, sauti yake, mikono yake na miguu yake ili tuwaambie wengine habari za upendo wake.
Jadili
Endapo ungepeta muda wa siku nzima na Yesu, ungemweleza nini? Ungeenda naye wapi?Ungefanya naye nini?
Omba
Muombe Yesu amtume mtu kwako ambaye unaweza kuueleza juu ya maneno ya hazina uliyoyapata humu.
Tengeneza
Fuatilia katika kujifunza mzunguko wa maisha ya kipepeo ama chura. Tambua mabadiliko makubwa yanayofanywa na nguvu ya Mungu.sisi nazi tunaweza na nguvu hii ikiwa tutaiomba na kuunganishwa na Yesu kupitia katika biblia.
JUMATANO
Novemba 07, 2018
BIBLIA INANIONESHA YESU
FUNGU: 21 Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.”
Inafurahisha kujua ni kwa nini tulipewa majina na yana maana gani. Jemma alifurahi kuwa jina lake katika lugha ya kifaransa humaanisha kito cha thamani na katika kiingereza humaanisha jiwe la thamani. Wakati mwana wa Mungu alikuwa azaliwe malaika wa Bwana walimtokea baba yake wa hapa duniani na kumwambia ataitwa Yesu .jina hili lilichaguliwa na Mungu mwenyewe maana atakuwa mkombozi wa ulimwengu.
Biblia imetumia majina mengi ya Yesu, na yote yanamdhihirisha jinsi alivyo, tabia yake na utume wake. Bibi alimwambia Jemma aende akachukue biblia yake, ili watafute majina mbalimbali ya Yesu. Waliandika majina yoote katika karatasi kubwa. Haya ni baadhi ya majina hayo.
Imanueli , mathayo 1:23: “23 Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi.”
Mungu hakutaka kuwa Mungu wa mbali, alitaka aishi kati yetu. Yesu alikuwa Mungu katika dunia hii.
Mwana wa Mungu, Yohana 3:16: “16 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”
Katika ubatizo wa Yesu mungu anatuthibitishia kuwa Yesu ni Mwana wake. “11 na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.”
( marko 1:11)
Mwana wa adamu, marko 10:45: “45 Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”Yesu alikua Mungu lakini alizaliwa na mwanadam, Mariamu. Hili tu linamfanya Yesu kuwa wa pekee maana alikuwa mwana wa mwanadamu na pia alikua mwana wa Mungu.
Neno, Yohana 1:1,14 “1 Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 14 Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.
Yesu alimdhihirisha Mungu kwetu.Alikua Neno la Mungu. Hapo mwanzo alitamka na vikawa!
“15 naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.
16 Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake.” (wakolosai 1:15,16) sio tu kwamba Yesu aliivuvia biblia, ambalo ni neno la Mungu kwetu sisi, bali Yesu ni neno la Mungu. Tukimjua yeye tumemjua Mungu.
Yapo majina mengine mengi ya Yesu katika Biblia. Waombe waalimu wako au wazazi wakusaidie kuyabaini.huu hapa ni mwanzo mdogo.
Mwana kondoo wa Mungu: yohana 1:29,36
Alpha na Omega: ufunuo 6:35
Mkate wa uzima: yohana 6:35
Jadili
Jua nini maana ya jina lako na ni kwa nini ulipewa jina hilo.
Omba
Muombe Mungu akusaidie uelewe majina yake ya thamanina maana ya majina yake yote unapojifunza neno lake.
Tengeneza
Andika majina ya Yesu katika vipande vya karatasi zinazolingana. Kisha tengeneza mnyororo wa karatasi alafu tundika katikati ya picha yako na ya familia yako.
ALHAMISI
Novemba 08, 2018
KUELEWA HAZINA YA MATUMAINI
FUNGU: “4 Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate kuwa na tumaini.”
Jemma alipenda sana shule, lakini alikuwa anatazamia sana likizo. Mwaka huu ilikuwa wasafiri kwa ndege kwenda kumtembelea bibi. Mama alinunua tiketi miezi kadhaa kabla ya safari, na jemma aliona kana kwamba likizo haifiki. Aliongea na bibi yake kwenye simu.
Bibi alijaribu kumtia moyo Jemma. Alimuelezea kuwa kutazamia jambo ni kuwa na matumaini. Unalipanga, unanunua tiketi,na unapanga nguo zako. Bibi yake naye alitamani kama likizo ingefika haraka. Bibi alimuahidi jemma kuwa angemkumbatia atakapotua katika uwanja wa ndege.
Bibi na jemma walizungumzia matumaini tunayopata katika biblia. Kwa kuwa Adamu na Hawa waliamua kumsikiliza shetani, warumi 1:25 hutuambia kuwa watu wakaanza kuabudu vitu vilivyoumbwa badala ya muumbaji. Watu wakaanza kufanya mambo mengi yaliyo maovu na yanayoumiza,huku wakipuuza kutumia muda wao kujifunza juu ya Mungu na kumuamini. Lakini kwa kuwa Mungu anatupenda sana alitengeneza mpango wa kuwaokoa wale watakaomrejea yeye. Mpango wa Mungu utamzuia shetani na dhambi kuwaumiza watu wake. Mwana wa Mungu, Yesu, angekuja duniani kama mtoto mchanga. Pamoja na kwamba Yesu hakuwahi kufanya jambo lolote baya ,alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, ili tusamehewe tuishi na Yesu milele. Upendo wa Mungu unatupatia tumaini kuwa tutakwenda mbinguni na kuishi naye milele. Bibi alimpa Jemma fungu kutoka katika hazina lisemali: “1 Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.
2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.
3 Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.” (Yohana 14:1-3)
Jemma alipokuwa akitafakari juu ya likizo , alitafakari itakavyopendeza Yesu atakapokuja mara ya pili. Alafu yeye na bibi watakuwa na Yesu milele. Ghafla Jemma hakuweza kutulia kwa ajili ya ujio wa Yesu. Alimpigia bibi yake simu na kumwambia. Bibi alifurahi kusikia kuwa Jemma alifurahia ujio wa Yesu. “Tunalo tumaini la ajabu, Jemma” alisema bibi. “ ni tumaini linaloufanya moyo wangu uimbe. Ni tumaini kuwa siku moja tutamuona Yesu mawinguni, na kisha atawaamsha wafu waliolala katika Bwana.”
“17 Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.” (1 wathesolonike 4:17)
Siwezi kuvumilia kusubiri!! Je wewe je?
Jadili
Unawezaje kulielezea tumaini hili kwa mvulana mwingine au msichana mwingine?
Omba
Muombe Yesu akusaidie umpe moyo wako kila siku, ili uweze kwenda naye atakaporudi mara ya pili.
Tengeneza
Tengeneza boksi la ahadi. Tengeneza boksi lingine dogo na ulipambe na stika na picha zingine. Kata makaratasi madogomadogo na uandike mafungu ya tumaini uyapendayo. Yaviringishe na kuyatumbukiza kwenye boksi mpaka lijae. Soma fungu mojamojakila siku ama umpe rafiki yako boksi la ahadi.
IJUMAA
Novemba 09, 2018
JEMA KUTOKA KWA BAYA – BIBLIA HUNISAIDIA KUONA TOFAUTI.
FUNGU: “30 nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.
31 Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.
Bibi alimuona Jemma akionekana kuwa na wasiwasi. Alimsikia akigombana na kaka yake katika mchezo waliokuwa wakicheza na kaka yake asubuhi ile. Maneno ya uchungu yaliongelewa. Mama alipomuomba aombe msamaha, jemma aliamua kufunga mdomo wake ili maneno yoyote yasitoke kinywani mwake. Hatimaye Jemma alikaa katika ngazi hapo njekwenye ngazi akiwa na huzuni nyingi.
Bibi alitambua kuwa kuna mafungu ya biblia mengi yanayoweza kumsaidia Jemma kuchagua lililojema na kufanya kilicho sahihi. Alimuomba Jemma avae miwani yake aliyotengeneza yenye maneno “Mungu ni pendo.” Kisha wakafungua biblia ya bibi na kuanza kuisoma huku wakizungumza.
Katika Marko 12 Yesu alisema kuwa amri kuu ni kumpenda Mungu wako kwa moyo wako wote, muda na kwa nguvu tulizonazo; na kuwa amri ya pili kwa ukuu ni kumpenda jirani yako kama nafsi yako. Bibi alimueleza Jemma kuwa ikiwa hatuna uhakika na kile tunachokihitaji kufanya, ni vyema tukatafakari kwanza, “natafakari namna ambavyo naweza kumpenda Mungu na kisha jirani yangu?” “Jemma,” aliita bibi “nina uhakika Yesu bado anampenda kaka yako na watu wote katika maisha yako, hata katika mtaa wako na mbali zaidi ya ujirani wako.”
“ikiwa unampenda kaka yako ,basi utajitahidi kusema maneno mazuri dhidi yake. Tunapoanza kuwa na hasira tutajizuia kuongea mpaka hasira ziishe. Ikiwa tunataka kumuheshimu mama katika pendo la Yesu tutamtii. Katika mithali 15:1 biblia inasomeka hivi “1 Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.”
Jemma alitafakari kidogo kisha akamfuata mama yake. Kulikuwa na maneno aliyotamani kuyatamka kama vile “samahani”.
1Yohana 2:3-8 hutuambia kuwa tunamfahamu Yesu ikiwa tutazishika amri zake, kutii neno lake na kutembea kama Yesu alivyotembea. Baadhi ya sheria hizi muhimu zilitolewa kwa wana wa Israeli kupitia kwa Musa na kwetu pia. Yesu aliziishi hizi sheria kumi. Za kwanza 4 zinatueleza namna ya kumpenda Mungu na za pili 6 zinatueleza namna ya kupendana sisi kwa sisi. Bibi alimsomea jemma hizo sheria 10 katika kutoka 20 na kumfundisha ili azielewe.
Bibi akasema, “Jemma kila mmoja hufanya makosa.lakini tunaweza kumuomba mungu msamaha, na kuwa na juhudi ya kuhakikisha tumeunganishwa na Yesu. Yesu aliahidi kuwa siku moja tutaishi na kupenda kama yeye anavyofanya. 1Yohana 3:2 hutueleza kuwa atakapodhihirishwa kwetu tutafanana naye. Wakolosai 3:12, “12 Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu,
13 mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.
Jadili.
Ni nini muongozo utakaokuongoza kujua kipi chema na kipi kibaya?
Omba
Muombe Mungu atusaidie kusema samahani kwa wengine tunapokosewa au kuwakosea.
Tengeneza
Andaa boksi la nguo.Katika nguo utakazoweka humo kila nguo iwakilisha tabia Fulani ya kibinadamu. Zingine zitawakilisha maneno yafuatayo; upole, kusoma biblia, kuomba, na zingine zitakuwa na maneno kama vile; kucheza gemu za video, kuwa mchoyo, kusema uongo, kuiba nk. Chambua nguo ambazo utaziandaa kwa ajili ya safari ya mbinguni na kuzikunja vizuri na kuzipanga kwenye sanduku.
SABATO YA PILI
Novemba 10, 2018
KUTIWA MOYO NA MANENO YA BIBLIA
FUNGU: “105 Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.
106 Nimeapa nami nitaifikiliza, Kuzishika hukumu za haki yako.
107 Nimeteswa mno; Ee Bwana, unihuishe sawasawa na neno lako.
108 Ee Bwana, uziridhie sadaka za kinywa changu, Na kunifundisha hukumu zako.
109 Nafsi yangu imo mkononi mwangu daima, Lakini sheria yako sikuisahau.
110 Watendao uovu wamenitegea mtego, Lakini sikuikosa njia ya mausia yako.
111 Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele, Maana ndizo changamko la moyo wangu.
Jemma alikuwa anajiandaa kusafiri kurudi nyumbani. Alifurahia kuwa kwa bibi yake na kutafuta hazina katika biblia. Atamkosa bibi yake waliyekuwa wakiongea naye mara kwa mara. Bibi yake alimueleza kuwa hazina walizokuwa wametafuta zimo ndani ya mioyo yao, na hivyo Jemma alikuwa anarudi nazo hazina hizi nyumbani. Jemma alikuwa na bib lia yake na alijua kuwa baba na mama watamsaidia kutafuta hazina nyingi zaidi.
Tunapohisi kuwa tumepotea na kutokuwa na uhakika ikiwa tumeunganishwa na yesu, tunaweza kuliamini neno la Mungu. Biblia ni kama mwanga unaotuonesha namna ya kuishi apendavyo Yesu.
Bibi alielezea kuwa ulimwengu huu sio nyumbani kwetu.Tunatazamia kwenda nyumbani. Kadiri ambavyo siku hii imekaribia ndivyo ambavyo watu watakataa kumpenda Mungu na kumfuata Yesu. Bila kuwa na hazina za biblia katika mioyo yao, wataona ni vigumu kuwa na huruma kwa wenzao na kusaidiana wao kwa wao. Ulimwenguni patakuwa mahali pagumu kuishi.
Yesu alisema kuwa yeye ni “nuru,” na kwama ni “njia, kweli na uzima,” (Yohana 14:6). Tunapounganishwa na Yesu kupitia katika kusoma biblia na kuomba, upendo wetu kwa Yesu utaimarishwa. Hatupaswi kuwa na wasiwasi juu ya maisha yetu. Hazina ya kweli ya biblia ni kwamba Yesu anatupenda. Mathayo 6:33, “33 Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”
Jemma alikumbuka juu ya kisa cha mwenye busara aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba, na mpumbavu aliyejenga juu ya mchanga. Dhoruba ilipowajia ni nyumba iliyojengwa juu ya mwamba tu ndiyo iliyosimama imara. Yesu alisema Yule mwenye busara alisikiliza maneno yake na kuyatumia maishani. Watu wengi husikiliza habari za Yesu na pendo lake, bali sio wote wanaopokea upendo wake kiasi cha kumuamini na kuishi kwa ajili ya Kristo.
Bibi alimueleza Jemma kuwa Yesu alihitaji awaambie wengine juu ya upendo wake na kufanya yaliyomema kwa watu wengine. “16 Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.” (Mathayo 5:16). Inafurahisha sana kuwa nuru ya Mungu kwa watu wengine.
“1 Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa;
2 mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato.”(Waefeso 5:1-2)Jadili
Taja hazina nane tulizojifunza katika juma hili.
Omba
Muombe Mungu akupe uelewa wa kina juu ya upendo wake kwetu.
Tengeneza
Tengeneza karatasi ndogo ya kuwekea alama kwenge biblia kisha andika fungu ulipendalo kutoka katika yale uliyojifunza juma hili. Lipambe hilo karatasi na stika au picha mbalimbali. Funga karibbon kazuri kanakoning’inia unapokuwa umefungua Biblia yako katika ukurasa unaosoma.