DIVISHENI YA AFRIKA MASHARIKI NA KATI
JUMA LA MSISITIZO WA HUDUMA ZA UWAKILI, 2017

MADA: “MAWE NDANI YA MFUKO WA KICHUNGAJI”

1 Samweli 17:48-49

Masomo haya yametayarishwa

Na

Mchungaji William K. Bagambe

Idara ya Huduma ya Uwakili na Huduma ya Amana

Divisheni ya Afrika Mashariki na Kati

 “YOTE KWA UTUKUFU WAKE”

 

SIKU YA 1

MAWE NDANI YA MFUKO WA KICHUNGAJI

1 Samweli 17:49: “Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi.”

Kisa cha Daudi na Goliathi katika Biblia ni moja ya visa vinavyomtahadharisha mtu wa kiroho kuhusu namna Mungu anavyofanya kazi na watu waaminifu waliojitoa kikamilifu, na hasa wale ambao wako tayari kutumia rasilimali zao kwa utukufu wa Mungu. Kwa ufafanuzi zaidi, ni dhahiri kwamba Daudi hakusukumwa na mwanadamu yeyote kumshambulia na kumwangamiza yule aliyekuwa tishio la Israeli. Wala hakusukumwa na ubinafsi; bali hatua aliyochukua katika lile shambulio ilitokana na heshima na utukufu aliokuwa nao kwa Mungu wa Israeli. Swali alilouliza linadhihirsha hatua hiyo, “…Mfilisti huyu asiyetahiriwa ni nani hata awatukane majeshi ya Mungu aliye hai?” 1 Samweli 17:26

Ukitazama nia ya Daudi kwa upana wake ilikuwa ni kukomesha ukosefu wa utii, dhihaka, laana, na kufuru ambazo Goliathi pamoja na Wafilisti wengine walikuwa wakitamka dhidi ya taifa takatifu la Israeli na Mungu mwenyewe. “Ikumbukwe kwamba utukufu na utakatifu wa Mungu unahifadhiwa na kuenziwa na washiriki wa taifa lake takatifu la Israeli, yaani Kanisa. Na wanafanya hivi wakitumia mibaraka Mungu aliyoweka mikononi mwao.” Wapendwa, tumieni mibaraka yake yote kwa utukufu wake. Daudi alikuwa na nia na mawe, alivyotumia kukabiliana jitu hili lisilotahiriwa.

Uwe mwangalifu kwa upeo wa ukubwa wako, ukichukulia mali, umaarufu, mafanikio kielimu, n.k. Cheo kubwa uliyo nayo pamoja na mafanikio haviwezi kukusaidia unapokabiliana na adui aitwaye Ibilisi. Unapojiona kuwa u mkubwa, adui yako anaweza kukulenga, kwa kupanga na kufanya jambo lolote hata kukutangazia kifo. Kwa bahati mbaya wengi wetu tunajivuna kwa mafanikio haya tukisahau kwamba tunayapata kwa utukufu wa Mungu na tunahitaji kuyahifadhi na kuyatumia kwa kusudi hilo. 1 Wakorinto 10:31 “Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.” Kinachotuumbua na kutuweka wazi kwa huyo adui yetu Ibilisi ni huko kujivuna.

Ukubwa wa umbile la Goliathi haukumsaidia Daudi alipoingia katika uwanja wa vita. Inawezekana kabisa kuwa ukubwa wa Goliathi uliamsha udadisi wa Daudi na hivyo kumchochea kushambulia. Kadiri ukubwa wako unavyoongezeka katika nyanja fulani, ndivyo inavyokuwa rahisi kulengwa au kushambuliwa. Mahali pekee unapoweza kuficha ukubwa wako ni chini ya mbawa zake. “Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu…” Matendo 17:28. Daudi alikuwa chini ya mbawa zake! Alimwambia yule Mfilisti katika 1 Samweli 17:45

“…Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la

Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.” Jambo la kufurahisha ni kwamba baada ya kauli hiyo inayoonesha dhamira thabiti ya Daudi, aliingiza mkono wake ndani ya mfuko wake wa kichungaji na kuchukua moja kati ya mawe matano yaliyokuwa ndani. Watu wanaofanya mambo yao kwa jina la Bwana wa Majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli, hufanya huku mikono yao ikiwa inaingia ndani ya mifuko yao, na kuchagua jiwe watakalotumia kushambulia adui. Hata baada ya maombi, ni budi mkono uingizwe ndani ya mfuko wa kichungaji wenye mawe kwa sababu hapo ndipo mibaraka ya Mungu inapotunzwa. Ni dhahiri kwamba maombi yanatangulia kutoa na kurudisha kwa Mungu.

Ni bahati mbaya tu kwamba baadhi ya watu wa Israeli kama vile mfalme Sauli, kaka yake Daudi aitwaye Eliyabu na wengine wengi walitamka kauli za kukatisha tamaa bila kujali mawe madogo yaliyokuwa kwenye kijito kile. Daudi akijitayarisha kwa ajili ya ile vita, kwa namna inayovutia hakuhangaika huku na huku kutafuta msaada au kuchangisha au kutangaza sadaka maalum. Alitumia mibaraka (au rasilimali) ambayo Mungu alikuwa amemjalia. Mawe, kombeo na utashi wa kushambulia, hivi vyote vyatoka kwa Mungu. Ni mpaka pale tutakapokuwa tayari kutumia mibaraka ya Mungu kwa utukutu wake ndipo majitu kama Goliathi yatakapokoma kututishia na kumkufuru Mungu. Tumia kile tu Mungu alichokubariki, ndicho anachoangalia.

Baada ya Daudi kutamka maneno, “Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.” 1 Samweli 17:45 aliingiza mkono wake na kuchukua moja ya mawe aliyookota kwenye kijito. Hii ni asilimia 20 ya rasilimali aliyokuwa ametayarisha kwa ajili ya utume wake. Tafadhali elewa kuwa ni asilimia 20 tu inayotosha kwa ajili ya utume. Daudi alikuwa na utume wa kupangua laana zote, kufuru na kashfa ambazo Wafilisti walikuwa wakitamka dhidi ya taifa takatifu la Israeli na Mungu mwenyewe. Jambo jema ni kwamba alibarikiwa kwa jiwe lile moja tu, kwani kitu pekee alichokuwa nacho ni mawe matano kwenye mfuko wake wa kichungaji.

Kanisa la Mungu lina utume wa kupeleka habari njema ya wokovu kwa kila taifa lugha na jamaa. Na hili ni agizo la Yesu Kristo mwenyewe. Tuwalete na kuwabatiza kwa jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. “Kipaumbele cha utume, ni wakati wa mavuno”. Hatuna budi kutambua kuwa katika kufanya hivi, tunakabiliwa na changamoto (ambazo ndio Goliathi kwetu). Goliathi wa nguvukazi ambao ni matumizi ya utawala wa kanisa, uendelevu wa miundombinu, kuhubiri na kushuhudia, na mengine mengi. Ni vema pia tukumbuke kuwa tunashindana dhidi ya mawimbi ya falme zinazotukandamiza, nguvu za yule mwovu. Goliathi hawa wanadharau, wanadhihaki, wanabeza na kusababisha changamoto kwa Israeli wa leo. Wakiuliza ikiwa tunaye Mungu tunayemwabudu. Kwa uhakika jambo hili limedumu kwa muda, baadhi yetu wanaogopa hizi changamoto na kwa sababu hii haya majitu (Goliathi) yanasimama mbele yetu bila kuguswa.

Sababu kubwa inayofanya haya majitu bado yamesimama ni kwamba mawe yale bado yapo ndani ya mfuko wa kichungaji. Hakuna anayeingiza mkono ndani ya mfuku kuchukua jiwe. Tumwigize Daudi, tuingize mikono yetu ndani ya mifuko na kuchukua jiwe moja katika yale matano ambayo Mungu ametubariki ili tuwapige Wafilisti tukianzia na Goliathi. Kanisa la Mungu linadhihakiwa na kufanyiwa kufuru, utukufu wa Bwana unakanyagwa kwa sababu mawe tuliyookota kwenye kijito bado tu yapo ndani ya mfuko wa kichungaji, mashambani, na kwenye bustani zetu. Hebu tuyachukue na kukamilisha utume wetu kwa jina la Bwana. Tunapata kigugumizi kanisani kwa sababu watu hawajaingiza mikono yao ndani ya mifuko. Mawe bado yametulia tu ndani ya mfuko wa kichungaji, na kadiri mikono inavyoendele kujizuia kuingia kwenye mifuko ya mibaraka, hawa Goliathi watabakia wakiwa wamesimama. Wapendwa muwe tayari kutumia kwa ajili ya utume kama Paulo katika 1 Wakorinto 12:15

Kufanya kitu fulani kwa ajili ya Mwenye Uweza maana yake ni kuingiza mikono mifukoni, kwenye akaunti zetu, mashambani mwetu n.k. kwani hapo ndipo mawe yetu yalipotunzwa. Chukua jiwe na kushambulia! Tumia mawe kupiga vipingamizi vyote vilivyo kati yako na utume wako. 1 Samweli 17:40 “Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao, maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti.” Daudi alikuwa na mawe matano ndani ya mfuko wake wa kichungaji lakini alitumia jiwe moja tu. Hii maana yake ni kuwa alitumia asilimia 20 tu ya mibaraka aliyokuwa nayo. Ikiwa tutamwiga Daudi, tutatenga asilimia 20 ya mapato yetu kwa ajili ya utume, yaani asilimia 10 Zaka ya Mungu na asilimia 10 sadaka ya Bwana. (10% sadaka inapendekezwa kulingana na kile Daudi alichotumia katika mbaraka). Kwa kufanya hivi, hatutakuwa na kina Goliathi badala yake tutapaa kama kanisa na utukufu wa Mungu utadhihirika.

Ellen G. White anasema, “kuna mali ya kutosha mikononi mwa waumini ya kuweza kutegemeza kazi bila kudhalilika ikiwa kila mmoja atafanya sehemu yake.” 5T 630. Anaendelea kusema kwamba, “Bwana kwa uweza wake ameagiza kwamba kazi katika shamba lake la mzabibu itegemezwe kwa mali iliyowekwa mikononi mwa mawakili wake. 3T 117. Wote tumeitwa kuunganika katika kuingiza mikono yetu mifukoni na kutoa mawe ili Goliathi apigwe na kuvunjwa vunjwa. (Kuhusisha washiriki wote katika kuchukua mawe kutoka kwenye mifuko). Wakolosai 3:23-24 “Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu, mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo.” Siku ambapo mawe yatachukulikwa kutoka kwenye mifuko, tutashangilia kwa shangwe kama wanawake wa Israeli walivyoshangilia kwa shangwe Daudi alipotenda.

1 Samweli 18:6-7 “Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake.” Wapendwa hatuna sababu ya kushangilia kwa shangwe wakati mawe yapo kwenye mifuko yetu, wakati fedha, mibaraka kutoka kwa Mungu Mwenyezi bado imefungiwa kwenye mabenki, wakati rasilimali zimefichwa na hakuna anayeziachia kwa ajili ya utume. Ufikie mfuko wako wa kichungaji na kuchukua mibaraka ili itumike kwa utukufu wa Bwana ambaye mibaraka inamiminika kutoka kwake.

Mafungu yafuatayo yasitumike kwa yeyote katika washiriki wa kundi la Mungu.

Yakobo 5:1-3 inaeleza kama ifuatavyo: "1 Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia. 2 Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. 3 Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho.”

Ufunuo 18:17 “kwa kuwa katika saa moja utajiri mwingi namna hii umekuwa ukiwa...” Hagai 1:2, 6, na 9

Imani ya Daudi ilikuwa katika Bwana, na alielewa hilo kutokana na uzoefu wake kwa uaminifu wa Mungu. Imani ya Daudi ilitokana na uzoefu wa neema ya Mungu na rehema zake katika maisha yake hadi wakati huo. Mungu alikuwa amemwokoa Daudi kutoka katika hatari mbali mbali hapo awali akithibitisha uweza na uaminifu wake, na kwa hiyo Daudi alimtegemea na kuamini atamwokoa kutoka kwa Wafilisti. Daudi alielewa kuwa uwezo haukuwa kwenye mawe au kombeo hata kama angetumia mawe yote matano bali uwezo ulikuwa kwa Bwana wa majeshi. Kama Daudi alivyoandika katika Zaburi 21:13 “Ee Bwana, utukuzwe kwa nguvu zako, Nasi tutaimba na kuuhimidi uweza wako.”

Vivyo hivyo uwezo haupo kwenye fedha tunayotoa au tunayorudisha kwa Bwana, bali uweza upo kwa Bwana wa majeshi mwenyewe, yeye anayetubariki kwa hiyo fedha. Jukumu letu ni kumheshimu kwa mali zetu, “Mheshimu Bwana kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote.” Mithali 3:9

“Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.” Kumbukumbu la Torati 8:18

Naam, uwezo upo kwa Bwana na wala sio kwa ile mali tunayompa kwa ajili ya utume. Lakini tunaporudisha kwa ajili ya utume, inakuwa dhahiri kwamba tumetoa vyote tulivyokuwa navyo kwake kwa dhati ili vitumike kwa ajili ya utume, ndiyo njia iliyo sahihi.

Tafadhali chukua jiwe kutoka kwenye mfuko wa kichungaji!

 

SIKU YA 2

Jukumu la Obadia.

1 Wafalme 18:3 & 12 3 Ahabu akamwita Obadia, aliyekuwa juu ya nyumba yake; (na huyu Obadia alikuwa mwenye kumcha Bwana sana); 12 Na itakuwa, mara mimi nikiondoka kwako, roho ya Bwana atakuchukua uende nisikojua; nami nitakapokwenda kumwambia Ahabu, naye asipokuona, ataniua, lakini mimi mtumishi wako namcha Bwana tangu ujana wangu.”

Mafungu mawili haya yanapotazamwa kwa muktadha wa kiroho, tunaweza kufikia hitimisho la haraka kwamba Obadia alikuwa mtu aliyemwamini Bwana. Alikuwa na uelewa kamili wa kuwa Mungu ni nani. Alimwabudu Mungu na kubakia mwaminifu kwake akitenda mema kwa kuwaficha manabii 100 katika mapango akiwalisha. Kitendo hicho cha kuficha manabii wa Bwana kilikuwa ni uhaini kwa taifa lile kwa wakati huo. Lakini kwa sababu kilifanyika kwa ajili ya Bwana, Obadia hakusita kukifanya. Uwakili na uaminifu vinaanzia katika kumwamini Bwana. Ni wale wanaomwamini Mungu kwa ukweli ndio tu wanaoweza kutenda ile iliyo haki. Inafahamika kuwa Yezebeli alipowauwa manabii wa Bwana, Obadia aliwaficha katika mapango mawili kwa idadi ya hamsini kwa hamsini na akawalisha kwa mkate na maji kwa kipindi chote hicho. Ni vigumu kupata upeo wa hali ya juu kiasi hiki cha uwakili katika watu wanaohudumu katika nafasi ya juu sana katika ikulu ya mfalme. Mfalme wa Wafalme, na Bwana wa mabwana. Ikulu ya Ikulu, lakini Obadia alifanya hivyo!

Kitendo cha kuwaficha watu mia moja kwenye mapango ukiwalisha chakula na maji kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu sio jambo jepesi. Inahitaji mtu awe mwaminifu na aliyejitoa kikamilifu ili kuweza kufanya hivyo. Wala jambo kama hilo haliwezi kufanyika kwa damu na mwili bali ni kwa Roho. Hii inaonesha kuwa Obadia alitumia mawe yote kwenye mfuko wa kichungaji na hakubakiza kwani sio rahisi ufanye kazi kubwa kama hii na mawe yabaki mfukoni. Ni lazima utakuwa umetumia yote kama Obadia alivyofanya. Atakuwa ameingia gharama kwa kulipia vyakula na mahitaji mengine. Upendo wa kweli na uaminifu vinahitaji uingie gharama na kulipia. Hauwezi kulisha na kunywesha manabii mia moja wa Mungu bila kuingia gharama. Jambo kama hili ndilo Mungu anatutaka tufanye, toa na kuwezesha.

Ni wakati wa kujiunga na kambi ya Obadia, watu wenye moyo uliotiwa hamasa na Mungu ili kuokoa maisha, watu walio tayari kuachia rasilimali zao, ambazo ni mibaraka kutoka kwa Mungu kwa ajili ya kuwapatia mema watu wake na hivyo kujenga ufalme badala ya kujenga majengo. Mungu anafurahia kufanya kazi na watu kama Obadia. Jaribu kufikiria jinsi Mungu alivyomwezesha Obadia kwa mibaraka ya rasilimali za kuweza kulisha watu mia moja kila siku. Mungu anayo namna ya kutubariki ikiwa hatutapoteza utambuzi wa chimbuko la hiyo mibaraka.

Eliya na Obadia, 1 Wafalme 18

1 Ikawa baada ya siku nyingi, neno la Bwana likamjia Eliya, katika mwaka wa tatu, kusema, Enenda, ukajionyeshe kwa Ahabu; nami nitaleta mvua juu ya nchi.

2 Basi Eliya akaenda ili ajionyeshe kwa Ahabu. Na njaa ilikuwa nzito katika Samaria.

3 Ahabu akamwita Obadia, aliyekuwa juu ya nyumba yake; (na huyu Obadia alikuwa mwenye kumcha Bwana sana;

4 kwa kuwa ikawa, Yezebeli alipowaua manabii wa Bwana, Obadia akatwaa manabii mia, akawaficha hamsini hamsini katika pango, akawalisha chakula na kuwapa maji).

5 Ahabu akamwambia Obadia, Pita katika nchi, kwenye chemchemi zote za maji, na vijito vyote; labda tutapata majani, tuwahifadhi hai farasi na nyumbu, tusipate hasara ya hao wanyama wote.

6 Basi wakaigawanya nchi, ili wapite katika nchi yote; Ahabu akaenda zake njia moja peke yake, na Obadia akaenda zake njia nyingine peke yake.

7 Na Obadia alipokuwa njiani, kumbe! Eliya akakutana naye. Akamtambua, akaanguka kifudifudi, akanena, Je! Ni wewe, bwana wangu Eliya?

8 Akamjibu, Ni mimi. Enenda, umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo.

9 Akamwambia, Nimekosa nini, hata unitie mimi mtumishi wako mkononi mwa Ahabu, aniue?

10    Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, hakuna taifa wala ufalme ambao bwana wangu hakutuma watu wakutafute; na waliposema, Hayupo, akawaapisha ule ufalme, na taifa, ya kwamba hawakukuona.

11  Nawe sasa wasema, Enenda, umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo.

12  Na itakuwa, mara mimi nikiondoka kwako, roho ya Bwana atakuchukua uende nisikojua; nami nitakapokwenda kumwambia Ahabu, naye asipokuona, ataniua, lakini mimi mtumishi wako namcha Bwana tangu ujana wangu.

13  Je! Bwana wangu hakuambiwa nilivyofanya hapo Yezebeli alipowaua manabii wa Bwana? Jinsi nilivyowaficha manabii wa Bwana, watu mia, hamsini hamsini katika pango, nikawalisha chakula na kuwapa maji?

14Nawe sasa wasema, Enenda umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo; basi, ataniua.

Mazungumzo kati ya Obadia na Eliya yanahitaji mtazamo wa kina

Kwanza maneno ya Obadia yanaonesha jinsi uelewa wake kumhusu Mungu ulivyokuwa mkubwa. Alifahamu jinsi Mungu alivyokuwa amefanya kazi na mtumishi wake Eliya aliyekuwa mwaminifu. Alielewa fika kwamba Mungu alikuwa amemhamisha Eliya kwa Roho wake na hivo anadhihirisha kwamba Mungu anaweza kuhifadhi wale walio wake kutoka kwa adui, na anapofanya hivyo, hakuna anayeweza kuwapata. Ni dhahiri pia kuwa Obadia alitambua jinsi Ahabu alivyokuwa anatisha. Ni katika uelewa huu ambapo Obadia alimwamini Mungu na kuthibitisha uaminifu wake. Ili uwe mwaminifu kwa Mungu ni lazima umfahamu vizuri. Uaminifu wa wengi wetu kwa Mungu ni mdogo kwa sababu tunaweka jitihada ndogo katika kutafuta na kufahamu kile ambacho anaweza kufanya. Ni katika hatua hii ambapo imani kwa Mungu inakua na kukufanya uwe mwaminifu. Hilo ndilo hitaji la uwakili. Katika upeo huu wa kiroho, mtu anaanza kujiuliza maswali kama, “Nimrudishie Bwana nini Kwa ukarimu wake wote alionitendea?” Zaburi 116:12

Hapo ndipo mtu anapojitambua na kuwa mkweli kwake mwenyewe huku akimfanya Mungu kuwa kitovu cha maisha yake. Muunganiko wetu na Muumbaji wetu unaweza kustawi tu katika mandhari ya kiroho kama hii, ndipo unapoweza kusema, “Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.” Zaburi 107:1. Leo hii sisi sote tunahitaji kufiki kimo hiki cha kiroho. Hebu Mungu na awabariki kadiri mnavyojiunganisha na Muumbaji wenu.

 

SIKU YA 3

 

MWANAMKE MWENYE KIJALUBA CHA MARHAMU

Yohana 12:3 3 Basi Mariamu akatwaa ratli ya marhamu ya nardo safi yenye thamani nyingi, akampaka Yesu miguu, akamfuta miguu kwa nywele zake. Nayo nyumba pia ikajaa harufu ya marhamu.”

Uchunguzi wa karibu na fasiri kadhaa za Injili zinatoa kile kinachoonekana kama hoja kadhaa za ushawishi wa utambulisho wa mwanamke huyu. Yohana anamtambulisha kwa jina la Mariamu. Waandishi wengine wa Injili wanamwita tu ‘mwanamke’. Jambo moja linaloonekana katika maandiko ya Injili zote ni kwamba huyu alikuwa ni mwanamke. Hiyo inatosha kwangu. Maelezo haya hayaendelezi jina la huyu mwanamke, hata hivyo umuhimu mkubwa upo kwenye alichomfanyia Yesu na wala sio katika jina lake. Dhana kuu ya uwakili ni kile ambacho mwenye dhambi anamfanyia Yesu baada ya kupokea ule uzoefu wa wokovu kupitia kwake.

Kwa kusudi la kusheheneza somo hili, nitachukua mafundisho yaliyopo kwenye Injili zote.

Kwanza kabisa mwanamke huyu hakukaribishwa kwenye chakula cha jioni. Hali yako inapokuwa mbaya kama ilivyo kwa wengi wetu, hauhitaji kusubiri kukaribishwa ili ufike pale Yesu alipo. Nenda tu; kwani - si ni yeye aliyesema, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” Matayo 11:28. Tafadhali mwendee leo ili akuponye ugonjwa wa kiroho wa ukosefu wa uaminifu. Ukifuatilia kile kilichofanyika kwenye ile meza ya chakula cha jioni, ni dhahiri kwamba yule mwanamke alikuwa anamfahamu Yesu fika. Akiwa na zawadi yake iliyokuwa ya thamni alienda moja kwa moja kwa Yesu na kujihusisha naye peke yake. Hakuoneka kumchanganya na mwingine yeyote, kumbe aliweza kumtambua mwokozi bila mashaka yoyote. Alitambua kuwa Yesu ni nani kwa jinsi alivyokuwa akionekana.

Jinsi Yesu alivyo dhahiri kwetu ni muhimu kwa sababu ndio msingi wa imani yetu kwa Mungu na Mwana wake ambaye ni mwokozi wetu Yesu Kristo. Katika maswala yenye asili ya kiroho na hasa katika uwakili, Mungu hawezi kuchanganywa na kitu au mtu mwingine yeyote. Taswira ya Yesu inaponasa katika fikra zako, kutoa na kumrudishia hakuwi tena mzigo kwako bali kunatiwa hamasa kiroho. Ikifikia hapa hakuna zawadi itakayoonekana ghali kumpa Yesu. Mwangwi wa imani katika Bwana unakuwa ni mkubwa kuliko kingine chochote. “Sauti ya imani yako inapokuwa ni kubwa kiasi hiki, hauwezi tena kusikia kile mashaka yanachosema”.

Hebu imani yako na iungurume.

Kilichofanya ile zawadi aliyoleta yule mwanamke isisimue ni ile harufu nzuri ya manukato iliyojaza nyumba nzima. Hakuna kinachoweza kutoa harufu nzuri ua uaminifu katika nyumba ya Bwana kama kumrudishia Bwana. Kumtolea Bwana kunatoa harufu nzuri ya manukato ya amani na uhuru ndani ya moyo wa mtoaji, inampatia uwezo wa kukua na kuenea katika nyumba yote ya Israeli wa kiroho. Unapoingia ndani ya kanisa linalomtolea Bwana hauwezi kukosa kusikia harufu nzuri ya manukato ya maombi, upendo, nguvu za kiroho na mwisho, ule utayari wa kumpokea Mwokozi atakapotokea mara ya pili.

Harufu nzuri kama hiyo haianzii nje bali huanzia ndani ya moyo wa mtoaji ambapo ndipo kilipo kiti cha ibada na upendo. Ile harufu nzuri iliyojaza nyumba ya yule Farisayo ilianza kujaza kwanza moyo wa yule mwanamke aliyetoa ile zawadi, na kumsukuma kumpa Yesu. “Kile kiujazacho moyo wa mtu ndicho kuijazacho nyumba anamoishi.” Unapoona kanisa kavu lililo maskini lakini kuna washiriki matajiri, mara moja unatambua kuwa mioyo yao pia imekauka na kuwa maskini na kukosa upendo kwa Mwokozi wao. Hali hii haitakiwi kuonekana au kujengwa ndani ya nyumba ya Bwana au ndani ya mioyo ya waumini.

Kama Biblia inavyoeleza, ile zawadi yenyewe ilikuwa ni ghali sana ikiwa imejawa na harufu nzuri ya manukato. Bila harufu nzuri kama hiyo, hakuna ibada! Kumbuka kuwa hata katika Agano la kale walitoa kafara ambazo zilichomwa ili kutoa harufu nzuri ya manukato kwa Mungu mbinguni: Mambo ya Walawi 1:9 “…lakini matumbo yake, na miguu yake, ataiosha kwa maji; na huyo kuhani ataviteketeza vyote juu ya madhabahu, ili iwe sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana.” Je, kutoa kwako au tuseme kurudisha kwako kunatoa harufu yoyote iliyo nzuri ya manukato kwenye nyumba ya Bwana au upo tu kufanya kinyume na hivyo?

Kwa haraka haraka unaweza kuona kuwa mtu pekee aliyeabudu kwa dhati ndani ya nyumba ya yule Farisayo alikuwa ni huyu mwanamke aliyekuwa na kijaluba kile cha manukato. Ni yeye pekee anayeonekana akitoa kitu kwa Bwana naye Bwana akapendezwa naye. Ni jambo la muhimu kwa Yesu kupendezwa na kitendo, hatua au njia unayoifuata. Hilo ndilo hitaji la pekee unalotakiwa kuonesha katika hii safari ya kiroho. Kupendezwa kwa Bwana kwa zawadi unayomtolea sio swala la thamani ya kile unachotoa, bali ni dhamiri ya kiroho iliyojengeka ndani ya zawadi hiyo. Hebu jenga dhamiri ya kiroho iliyo sahihi mbele za Bwana kila unapomtolea.

Katika kumimina manukato kutoka katika kile kijaluba, yule mwanamke ni kama alikuwa akisema “Sina ninachotazamia ila wewe, hakuna chenye thamani kwangu ila kukupenda, mimi ni wako.” Haya yote yanaonekana kusemwa na ile zawadi aliyoitoa. Kumtolea Bwana kunazungumza mengi ambayo yanayodhihirisha kuwa Bwana ni nani kwako. Moyo wako unaweza tu kuzungumza na Bwana kwa kumtolea. Yale manukato yalikuwa ghali sana. Inaaminika kuwa thamani yake kwa fedha ni kama mshahara wa kibarua wa mwaka mzima. Yote hayo yakamwagwa kwa Yesu katika ibada. Yesu anapokumwagia upendo na wokovu, hautaacha kupendezwa kwa kutoa na kurudisha, hiyo ndiyo njia pekee iliyo heri kwake. “Hauwezi kusema umemwabudu hadi hapo utakapoanza kutoa.”

Kuna dhana nyingi zilikuwa zinapita kwenye fikra za watu waliokuwa ndani ya ile nyumba ya yule mkaoma wakati yule mwanamke alipoingia. Mitume nao walilalamika kuhusu uharibifu uliofanywa na yule mwanamke mwenye dhambi. Hauwezi kuabudu katika mazingira yaliyojaa manung’uniko. Simoni ambaye ndiye mwenye nyumba mwenyewe alisemea mashavuni jinsi Yesu alivyokuwa akishughulika na yule mwanamke mwenye dhambi. Maoni ya Yuda nayo yalikuwa yamejawa upotovu na nia ya ubadhirifu. Nyumba ya Mungu imejawa na makundi yote haya. Wapo wengine kazi yao ni kunung’unika tu kuhusu kile wengine wanachofanya, wengine wapo tu kulaumu wengine, mbaya zaidi wapo ambao wamejawa na upotovu na nia ya ubadhirifu, wakiiba na kunyang’anya kile kilichorudishwa na wale wenye mioyo ya uaminifu kwa Bwana. Bahati mbaya makundi yote haya yanavuruga jitihada zote za uwakili zinazoanzishwa.

Hapo tena ukuaji wa kiroho unapunguzwa. Ni dhahiri kwamba katika hali kama hii hakuna ibada inayotendeka katika mazingira yaliyo hasi. Haiwezekani, Yesu hapendezwi na uumbaji wa namna hii na wala hana nia ya kutenda katika mpangilio huu. Wapendwa tumebanwa na mahangaiko tukitenda yasiyokuwa mema, tukikimbia haraka huku na huku katika njia isiyo sahihi. “Kuna haja gani kukimbia ikiwa hiyo njia sio sahihi?” Hii ni moja ya methali za Kijerumani.

Tamko na tendo la Yesu

Marko 14:6-9

6 Yesu akasema, (akiwaambia makundi yale) Mwacheni; mbona mnamtaabisha? Amenitendea kazi njema; 7 maana sikuzote mnao maskini pamoja nanyi, na kila mpendapo mwaweza kuwatendea mema; lakini mimi hamnami sikuzote. 8 Ametenda alivyoweza; ametangulia kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko. 9 Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake.”

Je, umeshawahi kutafakari maoni ya Yesu kumhusu huyu mwanamke katika mtazamo wa kiroho wa kutosha? Ninasisimka kwa jinsi Yesu alivyomtetea yule mwanamke dhidi ya wale waliokuwa wakimkashifu. Hii inadhihirisha jinsi Yesu alivyo mtetezi wetu nyakati tunapolaumiwa na maadui wetu. Yesu alitoa maoni chanya kumhusu mwenye dhambi kwa sababu alikuwa amemtendea kwa usahihi. Kumtolea Bwana ni kuzuri na kunakufanya uache urithi au alama inayoelezea uaminifu wako kwake. Yesu alisema, “Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake.” Kama Yesu angeongea kukuhusu wewe binafsi, unafikiri angetoa maoni gani? Je, Yesu anaweza kusema, “Amenitendea kazi njema?” Ili jambo hili litokee, ni lazima mawe yachukuliwe kutoka kwenye mfuko wa kichungaji. Kutoa kunaweza kujenga hadithi nzuri ya kiroho na urithi.

 

SIKU YA 4

MAWAKILI WAWILI KWENYE MAZISHI

Yohana 19:39-42 39 Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta machanganyiko ya manemane na uudi, yapata ratli mia. 40 Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika. 41 Na pale pale aliposulibiwa palikuwa na bustani; na ndani ya bustani mna kaburi jipya, ambalo hajatiwa bado mtu ye yote ndani yake. 42 Humo basi, kwa sababu ya Maandalio ya Wayahudi, wakamweka Yesu; maana lile kaburi lilikuwa karibu.”

Wengi wetu wanatambua jinsi gharama za mazishi zinavyoweza kuwa kubwa. Ni lazima pawe na sababu nzuri ya kuanza kufikiria gharama za mazishi, haitokei tu bali husukumwa na kujali, wajibu na upendo. Mkutano kati ya Nicodemu na Yesu usiku ule haukumwacha Nicodemu jinsi alivyokutana naye. Ilimfanya aanze kuangalia maisha kwa mtazamo mpya. Kwa hakika maongezi yalikuwa mazito kiasi kwamba Yesu alimwambia inabidi azaliwe upya. Ili sisi tuwe mawakili wa Bwana walio wema, hatuna budi kuzaliwa upya na kuwa na mguso na uhusiano wa karibu sana na Mwokozi na Bwana wetu Yesu Kristo. Wapendwa unapokutana ya Yesu uso-kwa-uso, fikra zikagongana, mioyo ikagusana, hauwezi kubakia yule yule. Utaanza kufanya kazi na Yesu; utakuwa unamfikiria bila kujali hali uliyo nayo, na muhimu zaidi utajiunga na klabu ya watoaji. Ni vigumu mtu kukutana na Yesu kiroho kisha asiwe mtoaji.

Kuna uthibitisho kwamba Nikodemu alipata neema. Alimwijia Yesu nyakati hizi za usiku akiwaogopa Wayahudi, lakini mwisho wa Injili, alinunua manemane na uudi yapata ratli mia ili kuupaka mwili wa Yesu (Yohana 19:39). Wakili wetu Mkuu alikuwa ameshafanya kazi yake na kuikamilisha. Alikuwa amemleta mwalimu wa Biblia katika ufalme wa Mungu. Mguso wa Yesu ulimbadilisha Nikodemu na kumfanya awe wakili. Hakubakiza jiwe ndani ya mfuko wake wa kichungaji. Alihakikisha hakuna namna ambayo watamkufuru Bwana wake ambaye amekuwa ni mwalimu na Mwokozi wake hata wakati ambapo alikuwa amekufa. Ilimpendeza Nikodemu kuifanya huduma ile. Sisi tulio waumini tunatakiwa kufikia upeo wa Yusufu na Nikodemu wa kutumia kile tulicho nacho kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Rafiki, Yesu ni mtoaji asiyeweza kufananishwa wala kulinganishwa na mwingine awaye yote. Ukisoma 1 Yohana 3:16 na Wagalatia 1:4 utagundua kuwa kule kuwa na mguso wa Yesu kunamfanya mtu kuwa mtoaji kwa sababu unakuwa umeunganika na mbingu ambayo ni chemchemi kuu itoayo. Kumtolea Bwana kwa uaminifu ni ushuhuda ulio dhahiri wa muunganiko wa mtu na mbingu.

Katika mtazamo wa kisheria alisulubiwa kama mwenye makosa ya jinai, unategemea huyo aliyetamkwa mhalifu angepata maziko ya namna gani? Labda mwili wake ungetupwa katika makaburi ya pamoja yaliyotengwa kwa ajili ya wahalifu. Ingekuwa ni hatari kuomba mwili wake aliyetamkwa ni mhalifu mwenye makosa ya jinai ili uzikwe kwa heshima. Ili uweze kupata mwili kama huo kwa ajili ya maziko ni lazima ruhusa ipatikane kutoka kwa mamlaka ingawaje pana uwezekano kuwa ni hatari kuomba ruhusa kwa hali kama hiyo. Viongozi wawili wa Wayahudi waliokuwa na ushawishi mkubwa walikuwa tayari kuchukua hatua hiyo. Mmoja wa hawa wawili aitwaye Yusufu wa Arimatayo alikuwa tajiri na maarufu akiheshimika sana, na mwingine ni Nikodemu. Hawa mawakili wawili waliokuwa wakuu katika jamii yao walichukua wajibu huu.

Baada ya kifo cha Yesu pale msalabani, Yusufu alimwendea Liwali Pilato na kuomba apewe mwili wa Yesu, naye Pilato akaridhia ombi hilo. Kuna mwanafunzi mwingine wa Yesu kwa siri aliyekuwa tayari kudhalilisha hadhi yake mchana ule. Huyu alikuwa Nikodemu. Siku moja usiku kabla ya siku hii ya huzuni Nikodemu alitafuta nafasi ya faragha ya kumhoji Yesu akihofu asionekane. Yusufu wa Arimatayo alikuwa anamiliki kaburi alilokuwa amelichonga mwambani pengine akipanga kuzikwa humo yeye mwenyewe. Hapo ndipo yeye na Nikodemu waliuweka mwili wa Yesu. Nikodemu akaleta mchanganyiko wa manemane na uudi uliokuwa wa gharama kubwa sana ili kutumiwa kuhifadhia mwili wa Yesu kwa ajili ya maziko. Manemane ni aina ya utomvu unaotumika kugundisha, na uudi ulikuwa na aina ya mafuta yanayonukia yaliyotumika kwa kusudi la tiba yenye harufu nzuri yanayotumika kwenye maziko ya wafu. Hawa watu wawili walifanya kazi pamoja wakiuwekea mwili wa Yesu mchanganyiko huu na kuzungushia nguo ya gharama aliyoinunua Yusufu. Hawa wawili walilipia gharama zote za maziko ya Yesu Kristo.

Waliuzungushia mwili ule nguo na kuufunika na mchanganyiko ule, kisha wakaongezea kuzungushia kichwa kwa nguo nyingine. Baada ya kuridhika kwamba wametayarisha vizuri ule mwili wa Yesu kwa ajili ya maziko, Yusufu wa Arimatayo akavingirisha jiwe kibwa penye lango la lile kaburi. Walitumia gharama hadi waliporidhika kwamba wamefanya kila kilichowezekana kwa ajili ya Bwana wao. Hii ni roho halisi ya uwakili. Hawa watu walidhihirisha wazi wazi kuwa walikuwa marafiki wa Yesu. Kitendo chao cha mwisho cha upendo kwake kimeorodheshwa kwenye Injili zote. Walihatarisha hadhi na heshima zao na zaidi ya hivyo ili kumfanyia rafiki wao maziko ya staha. “Upendo hutangulia kabla haujatoa katika kutumia”. Baadhi ya waumini waliokomaa katika neema wanasema, “Yesu ni kila kitu na wanaweza kufanya kila kinachowezekana kwa ajili yake kwa sababu alifanya kila kitu kwa ajili yetu.” Wote tunatakiwa kufikia upeo huu wa uaminifu. Na tufanye kila linalowezekana kwa utukufu wake.

Yusufu wa Arimatayo na Nikodemu hawakujua kwamba kwa kutenda kile walichotenda kwa wakati ule, walikuwa wanashiriki katika kutimiza unabii wa zamani uliotabiriwa na Isaya katika kitabu chake. Hii ilikuwa ni kadiri ya miaka 600 kabla ya kusulibiwa kwa Yesu ndipo Isaya aliandika kuwa, 8 Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. 9 Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.” Isaya 53:8-9.

Kutoa kwako au kutumia kwako kwa ajili ya Yesu kunaweza kuwa ni utimilifu wa unabii fulani

Kwa namna fulani inayofurahisha, Yesu hakubakia ndani ya lile kaburi kwa muda mrefu! Alifufuka kutoka kwa wafu siku tatu baadaye na yu hai milele. Ikiwa Yusufu na Nikodemu walitoa na kutumia kwa ajili ya Yesu wakati alipokuwa amekufa, je hatuhitaji kutumia zaidi kwake yeye mwokozi aliye hai? Ikiwa Yesu alipendezwa na kijaluba cha manukato kilicholetwa na yule mwanamke na kummiminia manukato, nina uhakika kuwa alipendezwa pia na kiwango kikubwa cha fedha walichotumia Yusufu na Nikodemu katika maziko yake. Ni dhahiri kuwa inagharimu leo hii kutumia kwa ajili ya Yesu Kristo, lakini marafiki wake watakuwa tayari kulipa gharama kwa neema ya Mungu. Ni kweli kwamba hawatasikitika.

Yohana 3:8

“Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho.” Wokovu unapoanza, wakati Yesu anapoingia ndani ya maisha ya mwenye dhambi, utasikia sauti ya huo wokovu, utaona matokeo ya wokovu, na utahisi huo wokovu. Utamwona mtu huyo akiwepo kwa ajili ya Yesu, utamwona huyo mtu akitoa na kumrudishia Yesu. Nikodemu na Yusufu ni mifano bora ya watu kama hao, nao hawataacha tu mawe ndani ya mifuko yao bila kuyatumia.

SIKU YA 5

 

ISRAELI WANATUMIA ZIADA YA BAJETI

Kutoka 36:5-7

5 nao wakasema na Musa, na kumwambia, Watu waleta vitu vingi sana zaidi ya hivyo vitoshavyo kwa ajili ya utumishi wa hiyo kazi, ambayo Bwana aliagiza ifanywe. 6 Basi Musa akatoa amri, nao wakatangaza mbiu katika marago yote, wakisema, Wasifanye kazi tena, mtu mume wala mwanamke, kwa ajili ya matoleo kwa mahali patakatifu. Basi watu wakazuiwa wasilete tena. 7 Kwani vile vitu walivyokuwa navyo vilikuwa vyatosha kwa kuifanya kazi hiyo yote, kisha vilizidi.”

Kisa hiki kinaanza pale Mungu aliposema, “Nao na wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao.” Kutoka 25:8

Tangu zama za kale, Mungu alitaka kukaa na kufanya kazi pamoja na watu wake (Israeli). Mungu anawabariki watu ili watumie ile mibaraka kufanya mapenzi yake na utume. Anahakikisha kwamba kila jukumu analotaka kukamilisha, atalikamilisha kupitia kwa mwanadamu. Natamani tutambue nia ya Mungu katika kufanya hivi. Nia yake ilikuwa akae kati yao, hata leo Mungu anataka uwepo wake uonekane kwa watu wake katika kufanya nao kazi. Ni dhahiri kwamba hauwezi kufanya kazi na Mungu bila kutumia, kwa sababu Mungu mwenyewe anatumia. Huko ni kutumia kulikobarikiwa, matumizi yenye mbaraka. Mara nyingi tunashindwa kutambua kwamba Mungu anapotuagiza kufanya jambo fulani linalohitaji kutumia au kutoa rasilimali tulizo nazo, nia yake ni kudumisha ule uhusiano uliopo kati yake na sisi na huko ndiko kukaa kati yetu. Hakuna kinachotuunganisha na Muumbaji wetu kuliko kurudisha au kutumia mibaraka aliyotujalia sawa sawa na jinsi alivyotuagiza. Kwa kufanya hivi tunabakia katka uwepo wa Muumbaji wetu na kuwa na mtazamo ulio sahihi.

Kwa hiyo anaposema turudishe zaka na sadaka, tumjengee hekalu na kutumia kwa utukufu wake, ni jambo la busara kwamba tunatakiwa kufanya kwa jinsi alivyoagiza. Kwa kufanya hivi tunabakia katika muunganiko na chimbuko la mibaraka, ambalo ni Mungu mwenyewe. Baada ya Mungu kumwagiza Musa kuwaambia Waisraeli wamjengee hekalu, Musa aliwaita Waisraeli na kuwaeleza yote aliyoagizwa, “Waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu.” Kutoka 25:2. Kumbuka wakati huo wana wa Israeli walikuwa jangwani na hakuna aliyekuwa ameajiriwa, wala kuwa na kipato cha namna fulani, lakini Mungu anawaagiza wamjengee hekalu ili akae kati yao. Watu walileta vitu alivohitaji Mungu. Je, walijengaje hilo hekalu? Hawa watu walitoa kile walichokuwa nacho. Siku zote Mungu anatutaka tutoe vile tulivyo navyo. Hawa watu kwa sababu walishiriki katika kutoa (Kushirikisha Washiriki Wote), walileta kwa ajili ya kazi ile hadi wafanya kazi wa madhabahuni wakamwambia Musa kwamba vilivyoletwa ni zaidi ya makadirio ya kazi ile.

Walitoa hadi pakawa na ziada. Wapendwa ni lini kanisa la Mungu litatambua dhana hii ya ibada? Badala yake, Israeli ya leo wana madeni! Madeni kanisani yamekuwa ni kawaida, je, tumepoteza mwelekeo wa kiroho? Kwa kweli ikiwa watu waliokuwa wakitangatanga jangwani, wasio kuwa na kipato chochote waliweza kutoa hadi wakawa na ziada ya makadirio, inakuwaje kwa Israeli ya leo yenye mawaziri, wabunge, wafanya biashara wakubwa, wana taaluma, wasomi, wahadhiri, wanaume na wanawake wenye hadhi kifedha, watu wanaoishi katika maeneo nyeti yanayozuiliwa, na wawekezaji wenye vitega-uchumi vinavyojitangaza.

Ni lini kanisa litakuwa na ziada katika makadirio yao kwa mfano ule wa kanisa wakati wa Musa? Ni nini kimetusibu watu wa kizazi hiki? Enzi za Musa watu walizuiwa wasilete kwa sababu vimetosha, lakini watu wa kizazi hiki wanashawishiwa kumtolea Bwana. Kuna tofauti, ni lazima uwe na mzungumzaji mwenye ushawishi mzuri ili mambo yaende. Leo hii mioyo ya watu imegandia kwenye vitu walivyo navyo kuliko zama za Musa. Utagundua kwamba Mungu aliwaagiza kutoa kwa mioyo yao yote, na agizo lake kwetu leo ni lile lile alilolitoa kwa wana wa Israeli. Usiachie mifuko na vichwa tu kutoa kwa Bwana, tumia moyo wako pekee, kwa sababu mioyo ndiyo inayomwelewa na kumfahamu Mungu. Labda sababu kubwa inayofanya tunashindwa kumtolea Mungu na kuwa na mapungufu kwenye makadirio yetu ni kwa kuwa bado tunatumia mifuko na vichwa vyetu kumtolea Mungu. Siku tutakapoanza kutoa kwa mioyo yetu yote kulingana na maagizo ya Mungu, tutakuwa na ziada ya makadirio yetu. Hakuna mawe yatakayobaki ndani ya mifuko yetu. Kumbuka kuwa mioyo pekee ndiyo inayoweza kuingia mifukoni na kuchukua mawe.

Wakati ule wa Musa watu walitoa vyote vilivyokuwa ndani ya mioyo yao, pamoja na ustadi wao hata na akili zao kwa sababu walijua kwamba vyote hivyo vilikuwa vimetoka kwa Mungu. “Basi Musa akawaita Bezaleli na Oholiabu, na kila mtu aliyekuwa na moyo wa akili, ambaye Bwana alimtia moyoni mwake hekima, kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza ili aende kuifanya kazi hiyo.” Kutoka 36:2. Wapendwa hatuwezi kumwomba Mungu atupatie mioyo aliyowapa Waisraeli nyakati za Musa? Ni moja ya kitu muhimu tunachohitaji sana hasa wakati huu ambao matukio ya dunia hii yanatuelekeza katika ule mwisho. Hapo ndipo tutakapochukua mawe kutoka kwenye mifuko yetu na kutimiza utume wa Mungu ili utukufu wake udhihirike.

 

SIKU YA 6

NAWE UKAFANYE VIVYO HIVYO

Luka 10:35-37

35 Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa. 36 Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang'anyi? 37 Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.

Wataalam kadhaa wa fasiri juu ya mfano uliotolewa na Yesu wa Msamaria mwema wametoa maoni yao na kuinua sauti zao. Wote wanakubaliana katika swala la upendo. Kwamba mpende jirani yako kama nafsi yako. Hii ni kweli isiyoacha mashaka, lakini tunaweza kusema kwamba mfano uo huo unaweza kuwa na mafundisho mengine pamoja na hili tunaloliongelea la kutoa na kutumia.33 Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, 34 akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. 35 Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.” Luka 10:33-35.

Huyu Msamaria alionesha upendo na huruma kwa yule mhanga wa unyang’anyi, lakini matokeo ya huo upendo na huruma yalidhihirika katika kutoa au kutumia baadhi ya rasilimali zake. Alitumia muda wake, nguvu, fedha na hata punda wake. Tunabarikiwa ili tuwahudumie wengine. Bahati mbaya ni yule Msamaria pekee aliyelifahamu hilo. Natamani watu wote wanaojiita watu wa dini wangeelewa jambo hili. Huo ndio uwakili katika upeo wake, au sivyo hali ya kiroho inavyomaanisha? “Upendo matokeo yake ni kutoa.” Maagizo ya Msamaria kwa mwenye nyumba ya wageni yanafurahisha. Alisema, “…Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.” Luka 10:35. Alikuwa tayari kulipa gharama zaidi. Natamani waumini tungechukua dhana hii ya kutoa kama Msamaria na kuifanyia kazi. Hapo ndipo tutakapokuwa na ziada ya makadirio yetu kanisani. Rafiki zangu, inawezekana.

Maana hasa ya upendo ni kutoa na kutumia. Jambo hilo ndilo mbingu ilifanya kwa wokovu wako. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Yohana 3:16. Paulo alitamka, “Nami kwa furaha nyingi nitatapanya, tena nitatapanywa kwa ajili ya roho zenu. Je! Kadiri nizidivyo kuwapenda sana, ninapungukiwa kupendwa? 2 Wakorinto 12:15. Yesu anahitimisha mfano huu kwa kumuuliza yule mwanasheria. Katika huo mfano ameorodhesha watu watatu: Kuhani, Mlawi, na Msamaria. Wawili wa mwanzo hawakumjali yule mhanga, ni Msamaria pekee aliyemjali.36 Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang'anyi? 37 Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.” Luka 10:36-37. Hauwezi ukawa mwema hadi hapo utakapotenda wema. “Hauwezi kuwa mwaminifu hadi hapo utakapotenda kwa uaminifu” William Bagambe

Wapendwa anachosema Yesu hapa ni hiki, “Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.” Uwakili kimsingi ni kutenda mema na kuwa mwaminifu na mkweli kwa Yesu Kristo na hasa kwa kile anachotegemea kutoka kwetu. Pale upendo wa Yesu utakapokuwa ndani yetu, tutajikuta tunatoa na kutumia kwa ajili ya utume kwani hatuwezi kunyamaza tu kana kwamba hatujaokolewa. “Maana, upendo wa Kristo watubidisha; maana tumehukumu hivi, ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote, basi walikufa wote.” 2 Wakorinto 5:14

Huu mfano wa Msamaria mwema ni kwa ajili yako.

 

SIKU YA 7

 

JITOE KWA BWANA KWANZA

2 Wakorinto 8:1-5

1 Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia; 2 maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao. 3 Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; 4 wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu. 5 Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu.”

Unaposoma mafungu matano haya ya waraka wa pili wa Paulo kwa Wakorinto sura ya nane, unagundua kuwa dhana kubwa ya kiroho inayojitokeza hapa ni kwamba waumini wa kanisa la Makedonia kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana. Ili uaminifu ujengeke ndani ya muumini yeyote wapendwa, ni lazima hiyo hatua ya kwanza itendeke. Kwanza itoe nafsi yako kwa Bwana. Katika maswala ya uwakili, ni Bwana kwanza, kisha hayo mengine yatafuata. “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Matayo 6:33.

Huo mfuatano wa kiroho ukifuatwa, basi kutoa kwa ajili ya kazi ya Bwana kutakuwa ndio mtindo wa misha yako hata wakati utafika ambapo usipotoa au kujihusisha katika shughuli za kutoa utajisikia kupungua kiroho na hivyo kutoa kilio kama kile cha wakazi wa Makedonia. Huu ndio mhimili wa ukomavu wa kiroho unaosiriba uhusiano wa mtu na Bwana wake. Hilo ndilo hitaji kubwa la nguvu na ukuaji wa kiroho. Mara nyingi tunashindwa katika majukumu yanayohusiana na safari yetu ya kiroho kwa sababu tumeweka jitihada kidogo katika kufikia lengo au wakati mwingine hatukuweka jitihada zozote.

Ukarimu wa watu wa Makedonia uliwezekana kwa sababu kwanza walijitoa kwa Bwana kisha kwa Paulo kama tunavyosoma katika fungu la 5. Jinsi ya kumtumikia Bwana ndilo lililokuwa dhumuni lao kubwa, ule udhati wa kujitoa kwao kwa Kristo kama Bwana wao. Kwa kutamani sana kumtumikia Kristo, hawakuruhusu hali nyingine yoyote ya kiuchumi iwazuie kujihusisha katika kazi yake. Ndiyo maana Paulo anazungumzia kwa ujumla kama huduma. (fungu la 4). Hayakuwa majukumu ya kifedha tu, bali ilikuwa ni fursa ya kuhudumia watakatifu – wale waliotengwa wawe mali ya Mungu. Ukarimu wetu unawezekana tu pale tutakapojitoa kwanza kwa Bwana. Kwa kufanya hivi, ndipo basi tunapokoma kuishi kwa ajili ya nafsi zetu bali kuishi kwa ajili ya Bwana ndiko kutakakokuwa ndani yetu kwani yeye ni mkarimu. Ukarimu wake unakuwa ndio wetu.

Watu wanapoinua viwango vyao vya kiroho kwa kujiunganisha kwanza na Bwana, ile haja ya kutoa inakuwa ndani yao. Hamu yao inakuwa ni kutoa kwa ajili ya kazi ya Bwana. Pale unapokuwa umewanyima fursa ya kutoa mara nyingi watakukumbusha na kuhimiza hadi watakapotoa. Ndivyo ilivyokuwa kwa kanisa la Makedonia. Umeshawahi kujiuliza kuwa ni lini ambapo kanisa lako litafikia upeo huu wa kiroho wa kujiunganisha na Bwana? Ikiwa iliwezekana kwa kanisa la Makedonia, inawezekana kwetu pia leo hii; tunachohitaji tu, ni kujitoa kwanza kwa Bwana. Paulo anasema, “3 Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; 4 wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu.” 2 Wakorinto 8:3-4

Watu walio chini ya neema ya Yesu kamwe hawawezi kuwa masikini. Siku zote ni matajiri na wakarimu. Paulo anashuhudia haya kwa andiko hilo hapo juu. Yesu alikuwa ndiye ukarimu wao. Kamwe usidai kuwa washiriki ni masikini kwani unapompokea Yesu katika maisha yako, ule ukarimu wake unageuka na kuwa wa kwako, kwa hiyo ikiwa wamempokea Yesu hakuna atakayesema ni masikini tena, Na ifahamike kwamba ukarimu unahusiana na kutoa kwa hiari kulingana na kile ulicho nacho. Mungu hahitaji mtu atumie au kutoa katika mibaraka ambayo yeye hana. Mungu anachotarajia ni kuona unatumia mibaraka aliyokupatia kwa utukufu wake.

 

SIKU YA 8

MWANAMKE MJANE WA SAREPTA

1 Wafalme 17:8-9

8 Neno la Bwana likamjia, kusema, 9 Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe.”

Chimbuko la kisa hiki ni ibada ya sanamu iliyoendelezwa na kukuzwa na Ahabu na Yezebeli. Kwa kweli hawa wawili mmoja akiwa mfalme na mwingine akiwa malkia hawakuwa wema. Ahabu akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana kuliko wote waliomtangulia. Nao wakawakosesha watu wa Israeli wamwache Bwana na kumsujudia Baali mungu jua ambaye alikuwa akiabudiwa na watu wa Sidoni. Siku moja Bwana alimtuma Eliya kwa Ahabu kumwambia, “Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.” I Wafalme 17:1. Sababu kubwa ilikuwa kwamba uovu umekithiri kati ya watu.

Huu ulikuwa ni wakati mgumu sana kwa Waisraeli. Badala ya mfalme kuwarudisha watu kwa Mungu, aliwaelekeza katika ibada ya sanamu. Hili ndilo jamba baya ambalo kiongozi wa taifa la Mungu anaweza kuwafanyia watu. Israeli katika utawala wa Ahabu wakazama katika ibada ya miungu. “Kila jambo linalotendeka kinyume na mapenzi ya Mungu ni uovu, kwa sababu haki ni kutenda lile lililo sahihi machoni pa Bwana.” William Bagambe

  • Mungu anasema katika Malaki 3:10 “Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.”
  • Yesu anasema katika Marko 1:44 “…akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao.”
  • Yesu anasema katika Matayo 23:23 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache.”
  • Neno la Bwana katika Kumbu kumbu la Torati 16:6 linasema, “ila mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako, apakalishe jina lake, ndipo mtakapomchinja pasaka jioni, katika machweo ya jua, kwa wakati kama uliotoka Misri.
  • Biblia katika Mithali 3:10 inasema, “Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya.”

Mafungu haya na mengine mengi yanasisitiza kumtolea Bwana. Ndugu zangu na dada zangu, ni wakati wa kumrudishia Bwana zaka na kumtolea sadaka ili kudhihirisha tunamheshimu kwa mali zetu na mazao ya mashamba yetu. Hayo ndiyo mapenzi ya Mungu. Ikiwa hatutafanya mapenzi ya Mungu, basi lolote tutakalofanya ni ibada ya miungu na kwa sababu hiyo ni uovu mbele za Bwana Mungu wetu. Kumbuka kwamba Israeli walipotenda uovu mbele za Bwana, alifunga mbingu na hapakuwa na mvua kwa miaka mitatu na nusu. Ninaamini kuwa Mungu anaweza kufanya jambo kama hilo tena.

Usisahau pia kuwa ni Mungu ndiye afunguaye mbingu ili kubariki mifuko yetu na akaunti zetu katika mabenki, ni yeye afunguaye mbingu kwa ajili ya mazao mashambani mwetu, ni yeye ambaye anatuwezesha kupata ajira. Hakuna mbaraka unaokujia usipoelekezwa kwako na Mungu. “Mtukuzeni Mungu ambaye kutoka kwake mibaraka yote yamiminika.” Lakini unapotenda uovu, Mungu anafunga mbingu na hivyo mibaraka yote inazuiwa. Naweza kukuhakikishia kuwa mifuko yako itakuwa mikavu kama mbingu, akaunti yako kule benki na mashambani kote kutakuwa na ukame, njaa itakuwa kwenye nyumba yako maisha yako yote. Kumbuka kuwa Mungu ni yule yule aliyekuwa akishughulika na Waisraeli. Ukame utakukumba ikiwa hautasikia na kutii wakati huu.

Mungu hutuma manabii wake kila wakati maovu yanapotendeka. Kwa hakika huu ujumbe unaousoma sasa unatoka kwenye maonyo ya nabii ukikutaka ufanye mapenzi ya Mungu katika maeneo ya kumrudishia Bwana kabla ukame haujakukumba. Mungu alimtuma Eliya kutanganza janga akisema, “Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.” 1 Wafalme 17:1. Huu ulikuwa nu ujumbe mgumu kupeleka na pia mgumu kuupokea. Bwana anapokutuma, ni vema kusema au kuandika vile vile Bwana alivyokuagiza.

Ni kweli kwamba mvua haikunyesha kwa hiyo miaka mitatu na miezi sita, kwa sababu ilikuwa ni sauti ya Mungu iliyotamkwa na Eliya. Wapendwa ikiwa tutaendelea kufanya maovu mbele za Bwana, mvua itakoma kwenye masanduku yetu ya fedha. Na hili neno ni dhahiri. Kwa sababu tumetenda uovu mwingi huku tukiendelea kupokea mibaraka, hakuna jambo lililobaki kwa ajili ya utukufu wake. Baada ya Eliya kufikisha ujumbe ule aliondoka. Ahabu akamtafuta lakini Mungu alikuwa amemficha. Ni neema kiasi gani ikiwa Mungu atakuficha! Mungu alikuwa na mpango mkubwa kwa ajili ya Eliya. Alimficha katika kijito cha Karithi na kumhudumia kwa chakula cha mkate na nyama kwa kutumia kunguru huku akinywa maji ya kile kijito. Mungu anaweza! Anaweza akakufanyia hivyo katika mazingira yoyote, hazuiliwi na kitu. Yeye ni Mungu.

Mvua haikunyesha kwa miaka mitatu na nusu, kukawa na ukame wa ajabu, njaa ikawa kali ikiandamana na adha zingine zinazojitokeza penye ukame. Vijito vyote na visima vikakauka, pamoja na kile kijito cha Kerithi ambacho Mungu alikuwa amembakizia Eliya. Hali ilikuwa ngumu na ikaonekana kama maisha yalikuwa yanakoma. Katika hali hiyo ya ukame, Neno la Bwana likamjia Eliya kusema, “Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe.” 1 Wafalme 17:9. 

Pana wakati ambapo kila kijito kinakauka, hata kile ambacho Mungu amekuelekeza. Lakini ukweli ni kwamba Mungu hajakaukiwa. Mhubiri mmoja alihubiri akisema, “Mungu anapofunga mlango, anafungua dirisha”. Ni kweli kwamba kijito cha Kerithi kilikauka, lakini Mungu alikuwa na rasilimali ndani ya mwanamke mjane wa Sarepta. Palikuwa bado panadondoka ndani ya nyumba ya huyu mwanamke mjane. Kwa Mungu sio kila sehemu inayokauka, katika baadhi ya nyumba bado kunadondoka, pamoja na nyumba yako. Chunguza nyumbani kwako ndugu yangu, chunguza nyumbani kwako dada yangu! Chunguza mifukoni mwako, kenye akaunti yako ya benki, shambani mwako uone kama mibaraka ya Bwana bado inadondoka. Hayo ndiyo mawe ambayo Bwana anataka uchukue kutoka kwenye mfuko wako wa kichungaji.

Mungu akamwambia Eliya, “…nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe.”

Jambo moja la kutambua hapa kumhusu Mungu ni kwamba, anapotubariki, anaagiza namna ya kutumia mibaraka hiyo. Ndiyo maana ni lazima kuwa makini tunaposikiliza sauti yake. Ikiwa ataagiza kwamba turudishe zaka ili kiwemo chakula nyumbani, basi inabidi kufanya hivyo. Msikilize kabla haujafanya kitu chochote. Mrudishie zaka yake kabla haujatumia fedha hiyo au kitu kingine chochote kinachohitaji kutolewa zaka kabla haujajifurahisha kwa fedha hiyo.

10 Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa. 11 Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. 12 Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. 13 Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. 14 Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi.” 1 Wafalme 17:10-14

Wapendwa, swala la uwakili linahusu Mungu kwanza, kisha wewe na jamaa zako. Ndivyo Eliya alivyomwambia yule mwanamke mjane. Mungu alimwambia Eliya, “Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe.” Lakini hakuonekana kama alikuwa ameagizwa kutenda chini ya uelekezi wa Mungu kwa kumpa Eliya chakula. Alitoa udhuru, mpaka Eliya aliposisitiza ndipo alipotenda sawa na maagizo.

Je, na sisi tunatenda kwa jinsi hiyo? Tunajitafutia udhuru kwa kusema tuna kidogo ambacho yawezekana kisitutoshe sisi wenyewe. Kwa Mungu hakuna misemo kama hiyo, kwamba ni kidogo au hakitoshi. Chochote ulicho nacho, kinatosha kwa kazi ya Mungu ya utume ikiwa utakitoa kwa upendo kulingana na maagizo ya Mungu. Uisikilze tu sauti yake na kutenda sawa sawa na maagizo yake. Kumbuka kwamba Mungu anajua dhahiri kile ulicho nacho, na kwamba ni kiasi gani kwa sababu kwanza kimetoka kwake kabla haujakipata. Kwa hiyo anaposema toa, au rudisha, anafahamu kwamba unatarajiwa kutoa kiasi gani. Ni pale unapokosa kutoa au kurudisha ulivyotarajiwa ndipo unapokuwa umetenda uovu.15 Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. 16 Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.” 1 Wafalme 17:15-16

Wapendwa fungu la kumi na tano linashangaza. Linasema yule mwanamke akafanya alivyosema Eliya. Kwa lugha nyingine alisikiliza sauti ya mbingu, na akatii maagizo na maelekezo yote kwa usahihi. Hatuwezi kuwa mawakili waaminifu mpaka tutakapojifunza kutii maagizo ya Mungu. Uwakili unahusu utii. Baada ya kutii na kumpatia Eliya, lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha. Unapotii maagizo ya mbingu, pipa lako wala chupa yako havitapungua! Amina. Badala ya hao watu wawili kula na kusubiri kufa siku ile, baada ya kutoa kulikuwa na chakula cha kutosha watu watatu kila siku hadi ukame ukafikia mwisho. Rafiki zangu hayo ndiyo ambayo Mungu anaweza kutenda. Anajua jinsi ya kutumia kile tulicho nacho, ikiwa tu tutamruhusu akitumie. Anaweza kukizidisha.

“Kutoa hakumfanyi mtu kuwa masikini, badala yake kunazidisha rasilimali alizo nazo.” William Bagambe. Jifunze hili kutoka kwa mwanamke mjane wa Sarepta. “Sio kutoa kunakoweza kukufanya masikini, bali ni umaskini wako wa kiroho ndio unakufanya usitoe.” William Bagambe. Kitendo cha utii wa yule mwanamke mjane kilikuwa sio cha kawaida, fikiria kilifanyika wakati wa Eliya, lakini Yesu anakirudia wakati wake kule Nazareti. Hivi ndivyo asemavyo katika Luka 4:25-26 “25 Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; 26 wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Maana yake ni kwamba ingawaje miaka mingi ilikuwa imepita, Yesu alijua kile kilichotendwa na yule mwanamke mjane

Je, una uhakika Yesu anajua utiifu wako, utoaji wako, jinsi unavyorudisha? Ni budi ajue. Je, utaingiza mkono wako ndani ya mfuku uchukue mawe?

MUNGU NA AKUTUNZE KATIKA VIGANYA VYAKE VYENYE UPENDO

AMINA

“YOTE KWA UTUKUFU WAKE”